1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzanian yafungua milango yake kwa wawekezaji wa madini

Amina Mjahid
22 Februari 2021

Serikali ya Tanzania imewafungulia milango wawekezaji wakubwa na wadogo katika sekta ya madini ikisema imezifanyia marekebisho baadhi ya sheria zake kwa lengo la kutoa manufaa kwa pande zote.

https://p.dw.com/p/3piZB
Tansania Miner zum Millionär | Saniniu Laizer
Picha: picture-alliance/AP Photo

Katika kongamano la kimataifa la madini linaloendelea mjini Dar es Salaam, washiriki kutoka nchi 24 wanaojumuika katika kongamano hilo la kimataifa la uwekezaji katika sekta ya madini wamejulishwa namna sekta  hiyo ilivyopiga hatua hasa wakati huu ambako kunatajwa kuendelea kugunduliwa madini ya aina mbalimbali.

Wawekezaji hao ambao baadhi yao wamelazimika kushiriki kwa njia ya video kutokana na janga la corona, wamefafanuliwa kuhusu sekta hiyo inavyoendelea kuchanua siku hadi siku huku wakihakikishiwa kuendelea kushirikiana na serikali kuzitafutia majawabu changamoto zote zinazogusa sekta hiyo.

Wakati wa nasaha zake katika kongamano hilo la siku tatu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani aliahidi kutowatupa mkono wawekezaji wa aina yoyote watakaokuwa na kiu ya kuingia kwenye sekta ya madini nchini Tanzania.

Mchimba madini wa Tanzania apata jiwe jingine kubwa la Tanzanite

Bi Suluhu amesema makongamano kama haya yanafungua milango katika ya sekta binafsi na serikali ya kuwa na majadiliano yanayoweza kuridhiwa na pande zote kuhusu mapato yatokanayo ya sekta hii.

Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa matatu barani afrika inayozalisha kwa wingi madini ya dhahabu katika miaka ya hivi karibuni ilianzisha majadiliano na makampuni ya nje yanayofanya shughuli zake nchini, ambayo yalihitimisha kilio cha muda mrefu cha kugawana mapato ya bidhaa hiyo sawa kwa sawa na kampuni ya Barrick.

Mengi yamefikiwa katika kuleta unafuu wa kodi kwa wachimba madini

Tansania Samia Suluhu
Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Ingawa mchango wa sekta ya madini unatajwa kuwa wa wastani siyo kama ilivyotarajiwa, hata hivyo waziri wa sekta hiyo Dotto Biteko anaamini kuwa bado kuna mengi yamefikiwa katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa juhudi za ubadilishaji wa sheria zilizosaidia kuleta unafuu wa kodi kwa wachimbaji wadowadogo na wale wakubwa.

Makongamano kama haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka kama jukwaa la kujadiliana na kupeana mikakati mipya ya namna ya kuisukuma mbele sekta ya madini.

soma zaidi: Maziwa makuu wakubaliana kuhusu madini

Mataifa ya afrika yanaona kuwa huu ni muda muafaka makongamano kama haya yanayojadili rasilimali zinazopatikana afrika yakafanyika katika maeneo ambayo utajiri huo unapatikana.

Ingawa mataifa hayo yamebarikiwa kuwa na rasimali za aina mbalimbali, mengi yanaendelea kushuhudia anguko la uchumi kwa sababu raslimali hizo zinachangia kwa kiwango kidogo katika maendeleo. 

Mwandishi George Njogopa