1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taswira ya Uislamu yawachanganya Wajerumani

Daniel Heinrich/Mohammed Khelef16 Desemba 2014

Vuguvugu linalopinga kusilimishwa kwa Ujerumani, Pegida, sasa limekuwa zaidi ya jina la maandamano ya kawaida, kwani Ujerumani yenyewe imeelemewa na watu wengi wenye khofu dhidi ya Uislamu.

https://p.dw.com/p/1E5Pa
PEGIDA-Demonstration in Dresden
Picha: Reuters/H. Hanschke

Kuna hisia za kuchanganyikiwa na zisizo mashiko lakini ambazo zinachochewa na masuala kadhaa: kutokea mashambulizi ya Septemba 11 na khofu ya daima dhidi ya Uislamu, mijadala juu ya kofia na maburka, upandikizaji wa siasa kali za Dola la Kiislamu (IS), ambapo Waislamu wa Kijerumani wenye asili za kigeni wamekwenda kujiunga nalo kama wapiganaji wa jihadi, wimbi la wakimbizi kutoka nchi ambazo zinakabiliwa na IS, na suala lililochukuwa muda mrefu la ikiwa nchi yenye Waislamu wengi Uturuki, iruhusike kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ama la.

Watu wengi wameelemewa na hayo na hilo linaweza kufahamika, kwa sababu ukiacha uchambuzi wa kisomi kwenye siasa na vyombo vya habari, watu wengi hawana uwezo wa kuchambua tafauti kati ya taswira hiyo inayombatanishwa na Uislamu na Uislamu halisi. Kwao wao kila Muislamu ni kama Muislamu mwengine.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vinazidi kuzifanya hisia hizo kuwa kali. Mfano halisi ni tukio la hapo jana la mkahawa kutekwa nyara mjini Australia. Hata kabla ya taarifa za ndani kujuilikana, tayari habari nzima ilishapagazwa majina yale yale: "jihadi", "mpiganaji wa Mungu", "Muislamu mwenye siasa kali." Hakuna maneno ya kutafautisha ukweli mmoja kutoka mwengine. Na katika hali ya kawaida, hilo linachanganywa na kauli ya hivi karibuni ya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki, ambaye aliwashauri Waturuki wanaoishi hapa Ujerumani kutojiona Wajerumani sana.

Daniel Heinrich
Daniel HeinrichPicha: DW/M. Müller

Ukimya katika mambo muhimu

Kwayo pia zikaja ripoti juu ya vijana kutoka Wuppertal waliokuwa wakijiita "polisi wa Sharia" ambao wakitembea mjini na kuwataka watu wavae mavazi sahihi ya Kiislamu. Upumbavu wa kiasi gani! Na kipi zaidi ya "Uislamu ni uovu" ambacho raia wa kawaida anaweza kukisema katika hali kama hiyo?

Tatizo la Ujerumani ni kwamba kuna watu wengi wanaoyahofia hayo lakini hakuna mjadala wa wazi kwayo. Na watu wengi, kwa hivyo, wanajihisi kwamba hisia zao hazipewi uzito. Badala yake wanabezwa hata kwenye kiwango cha watunga sera. Mfano wa karibuni ni kauli ya Waziri wa Sheria wa Ujerumani, Heiko Maas, ambaye ameyaita maandamano ya Dresden kuwa ni "aibu kwa Ujerumani".

Kauli hii ni ishara mbaya kabisa ya kuwatenga watu na inaonesha kwa kiasi gani namna uwelewa wa jambo hili ulivyopewa umuhimu mdogo, kwani hata kwenye chama chake Maas mwenyewe, kuna sauti nyingi zinazounga mkono mawazo ya Pegida.

Asilimia 46 ya walioulizwa kwenye chama hicho cha SPD walisema wanaakisi matakwa ya Pegida. Wanasema kuwa SPD si chama ambacho hisia za waumini wa Ukristo zinazingatiwa. Na hilo ni jambo la kufanyiwa kazi, maana matokeo yake ni kwamba makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia yanaweza kuwavutia wengi miongoni mwa raia.

Mwandishi: Daniel Heinrich
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Elisabeth Shoo