1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Iran yapuuza miito ya kuwaachilia mabaharia wa Uingereza

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDL

Iran leo imepuuza shinikizo la kimataifa linaloitaka iwaachilie huru mabaharia saba na wanajeshi wanane wa Uingereza. Badala yake imesema Uingereza inatakiwa ibadili tabia yake juu ya mgogoro huo ambao umekuwa ukiendelea kwa siku tisa sasa.

Iran iliwakamata waingereza hao 15 mnamo tarehe 23 mwezi uliopita ikiwatuhumu kwa kuingia eneo la bahari lililo himaya ya Iran bila kibali.

Rais wa Marekani George W Bush amewaeleza mabaharia saba na wanajeshi wanane wa jeshi la maji la Uingereza kama mateka na kusema tabia ya Iran kuendelea kuwazuilia haiwezi kusameheka. Bush ameitaka Iran iwaachilie huru wanamaji hao.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amejibu matamshi ya rais Bush kwa kuzieleza dola kuu duniani kuwa kaidi kwa kushindwa kuomba msamaha juu ya kile anachokiita hatua ya mabaharia wa Uingereza kuingia katika eneo la bahari lililo himaya ya Iran.

Mgombea wadhifa wa urais nchini Ufaransa, Segolene Royal, leo amependekeza Umoja wa Ulaya uiwekee vikwazo Iran kwa kuwazuilia wanamaji hao wa Uingereza.