1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN:Iran ina makombora mapya ya masafa marefu

22 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBNb

Iran imetangaza kuwa na makombora mapya ya masafa marefu katika maonyesho ya kila mwaka ya kijeshi ili kuadhimisha miaka minane tangu kuingia vita na Iraq.Kombora la Ghadr ni kombora lake la zamani la Shahab la masafa marefu lililoimarishwa na kuwa na uwezo wa kusafiri hadi kilomita 1300.

Iran inakabiliwa na shutma kutoka jamii ya kimataifa kuhusu mpango wake wa nuklia unaozua utata.Mataifa ya magharibi yanaamini kuwa mpango huo huenda ukatumika kutengeza silaha za nuklia jambo ambalo Iran inakanusha.Marekani na Israel hawajakanusha uwezekano wa kuiadhibu Iran kwa kushikilia kuendelea na mpango wake wa nuklia.Iran kwa upande wake inashikilia kuwa haina mpango wa kushambulia nchi yoyote ile ya kigeni ila kuonya kuwa endapo itashambuliwa italipiza kisasi.

Malori ya kijeshi katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye madhabahu ya Ayatollah Ruhollah Khomeini yalibeba mabango yanayoshtumu Marekani na Israel na kutoa wito wa kuondolewa kwa taifa la Israel.Mapema kamanda mmoja wa jeshi la angani la Iran alisema kuwa jeshi limeandaa mpango wa mashambulizi endapo Israel inaivamia kwasababu ya mpango wake wa nuklia.

Kauli hiyo inatolewa baada ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner kuonya kuwa ulimwengu sharti ujiandae kwa vita ikiwa Iran inaendelea kukiuka vikwazo vya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa vya kusitisha mpango wake wa nuklia.