1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tendai Biti ateuliwa Waziri wa Fedha Zimbabwe

P.Martin - (RTRE)10 Februari 2009

Zimbabwe,kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai amemteua Tendai Biti kuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya umoja wa kitaifa. Amesema,lengo lake ni kuleta utulivu wa kiuchumi na kuvutia vitega uchumi kutoka n´gambo.

https://p.dw.com/p/Gr2i
***MDC-Generalsekretär Biti: In Simbabwe herrscht Krieg, Abs*** Zimbabwe's opposition party Movement for Democratic Change (MDC) secretary-general Tendai Biti speaks at a news conference in Johannesburg, Sunday, April 20, 2008. Biti, said that said violence since March 29 elections had forced 3,000 families out of their homes. Hundreds of people had been hospitalized with injuries and ten people killed. (AP Photo/Bram Lammers - DAILY TIMES) ** SOUTH AFRICA OUT **
Tendai Biti alieteuliwa kuwa Waziri wa fedha wa ZimbabwePicha: AP

Tendai Biti Katibu Mkuu wa chama cha Movement for Democratic Change MDC atakuwa na kazi ya kuujenga upya uchumi wa Zimbabwe ulioharibika na kurejesha imani ya wafadhili wa magharibi. Muda mfupi baada ya kumteua Biti kuongoza wizara ya fedha, Tsvangirai aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Harare, kuwa kazi ya wizara ya fedha itakuwa kujenga mazingira ya kiuchumi yaliyo imara kwa Wazimbabwe wote na kuifanya Zimbabwe kuwa mahala imara pa kuwavutia wawekezaji.

Tsvangirai aliekubali juma lililopita kuunda serikali ya muungano pamoja na Rais Robert Mugabe,baada ya ugomvi wa miezi kadhaa,ataapishwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe siku ya Jumatano kuambatana na makubaliano ya kugawana madaraka.Lengo la makubaliano hayo ni kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo na kufufua uchumi ulioharibika.Baraza zima la mawaziri litaapishwa siku ya Ijumaa.Kiongozi wa chama cha MDC amesema, wanafahamu kuwa serikali ya umoja si suluhisho kamilifu lakini vile vile wanatambua uwezekano wa kushughulikia mahitaji ya umma.

Wachambuzi wanaamini kuwa Mugabe na Tsvangirai,mahasimu wawili wa zamani,wakilazimika kufanya kazi pamoja,watawachagua washirika wao wa kisiasa,badala ya wataalamu na wanauchumi wenye ujuzi bora zaidi kuijenga upya nchi.Kuchaguliwa kwa mwanasheria Biti- mwanachama muasisi wa MDC aliepinga kuafikiana na Mugabe,huenda kukaimarisha maoni kama hayo. Vile vile kuna hatari ya mvutano kuzuka kati ya Biti na Gavana wa Benki Kuu Gideon Gono alie mshirika wa Mugabe.Kwani waziri wa fedha akiwa pia naibu wa Gavana wa Benki,Biti atalazimika kufanya kazi pamoja na Gono.Na hiyo huenda ikawa changamoto yake kubwa anasema Susan Booysen alie mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Witwatersand.Anasema,Biti ni mtu mwenye elimu ya juu,ni mwerevu kisiasa na akifanikiwa katika wadhifa aliopewa,basi chama cha MDC kitanufaika katika kampeni za siku zijazo na atauvutia umma.