1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko katika uchaguzi lawatisha wanasiasa mjini Berlin.

Stützle , Peter (DW Berlin)29 Septemba 2008

Katika uchaguzi jimboni Bayern jana Jumapili chama cha CSU kimeshindwa kulinda wingi wake bungeni.

https://p.dw.com/p/FR69
Mwenyekiti wa chama cha CSU Erwin Huber (k) akizungumza na viongozi wengine wa chama hicho pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika kampeni za chama hicho katika uchaguzi wa jimbo la Bayern hivi karibuni.Picha: picture-alliance/ dpa


Katika uchaguzi jimboni Bayern jana Jumapili, chama cha CSU ambacho kwa muda wa miaka takriban 46 kilikuwa kikitawala peke yake kimeshindwa kulinda wingi wake bungeni. Kimepata kiasi cha asilimia 43.4 tu. Kundi ambalo halikuwa likiwakilishwa katika bunge la wagombea wa kujitegemea limepata zaidi ya asilimia kumi na kwa sasa ni kundi la tatu lenye nguvu katika jimbo la Bayern nyuma ya chama cha Social Democratic, SPD, ambao wamepata asilimia 18.6 ikiwa ni matokeo mabaya kabisa katika historia ya chama hicho.



Chama cha Kiliberali kwa upande wake kimepata asilimia 8 ikiwa ni matokeo mazuri kabisa kwa chama hicho hadi sasa na matokeo hayo yamekuja baada ya kutoweka kwa muda mrefu chama hicho katika bunge la jimbo hilo. Chama cha walizi wa mazingira , Greens, kimepata asilimia 9.4 ambayo ni matokeo yake bora kabisa katika jimbo hilo la Bayern, chama cha mrengo wa shoto , Linke kimepata asilimia 4.3, ambapo kutokana na utaratibu wa kuwa chama lazima kipate asilimia kuanzia tano hakitawakilishwa katika bunge la jimbo hilo.

Mabadiliko hayo yaliyoletwa na wapiga kura pia yanaathari siasa za Ujerumani mjini Berlin.

Ile hali ya chama cha CSU kupata wingi wa kura iliyoonekana kama ni sheria ya msingi , haiko tena na chama cha CSU ni lazima sasa kitafute mshirika ili kuunda serikali ya mseto, hali iliyokuwapo tu katika jimbo hilo la Bayern katika miaka ya 50.

Tetemeko hili limefika hadi mjini Berlin. Angela Merkel anataka baada ya uchaguzi mkuu kubakia kuwa kansela, lakini si kwa kushirikiana na chama cha Social Democratic SPD , lakini na chama cha kiliberali. Lakini si tu chama cha FDP kinatakiwa kuwa na nguvu zaidi , lakini pia vyama ndugu vya CDU na CSU vinapaswa navyo kuwa imara.

Lakini katika uchaguzi huu wa jimbo la Bayern vyama hivyo vimefanya kinyume chake, vimeanguka kwa mshindo mkubwa.

Pamoja na hayo mgombea wa kiti cha ukansela kwa tikiti ya chama cha Social Democratic aliyeteuliwa hivi karibuni Frank-Walter Steinmeier tetemeko hili halikumuweka mahali salama.

Marafiki zake wa vyama vingine katika jimbo la Bayern wamefanikiwa, licha ya udhaifu wa CSU .

Hata iwapo angependa kushirikiana na vyama vya Greens na FDP, muungano huu unawezekana tu iwapo, chama cha SPD kitakuwa imara zaidi, na kwa hivi sasa kinaonekana kuwa dhaifu kidogo.

Matokeo haya ya uchaguzi wa Bayern yameonyesha kuwa kuna kuporomoka kwa vyama vikuu nchini Ujerumani , vyama ndugu vya CDU na CSU na SPD vimeendeleza kuporomoka huko tangu chaguzi zote za miaka iliyopita kama uchaguzi wa mwaka 2005 ulivyoonyesha.

Hata hivyo umuhimu ni kuwa kuboronga huko bado hakujabadilika. Wapiga kura wa chama cha SPD ambao hawaridhishwi wamejipeleka katika chama cha mrengo wa shoto cha Linke, na wengine kwa chama cha Greens, wale ambao hawaridhishwi na mambo katika chama cha CDU/CSU wamekipigia chama cha FDP na baadhi wakapiga kura kwa wagombea wa kujitegemea.



►◄