1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa ya tetemeko la ardhi.

Abdu Said Mtullya1 Oktoba 2009

Watu zaidi ya 500 wamekufa kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi katika kisiwa cha Sumatra.

https://p.dw.com/p/JvV4
Maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika kisiwa cha Sumatra.Picha: AP

Watu 529 wamekufa kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi katika kisiwa cha Sumatra, nchini Indonesia. Maafisa wa serikali wamesema wanahofia idadi ya watu watakaokufa itaongezeka. Waokoaji wanatumia mikono mitupu kujaribu kuwafikia watu walionaswa chini ya vifusi.

Wakati ndege zilizokuwa na shehena za misaada zilipokuwa zinaanza kuwasili katika kisiwa cha Sumatra, tetemeko lingine kubwa lilitokea kusini mwa kisiwa hicho na kusababisha kiherehere miongoni mwa wakaazi.

Tetemeko la jana alasiri lililofikia nguvu ya 7.6 liliteketeza majumba na kusababisha moto katika mji wa Padang wenye wakaazi karibu milioni moja.Kwa mujibu wa idara za serikali watu 529 wameshakufa na wengine105 wamejeruhiwa. Lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Mkuu wa kitengo cha maafa kwenye wizara ya afya, Rustam Pakaya, ametabiri kwamba maalfu wengine watakufa.

Tetemeko hilo lilizikumba fukwe za kisiwa cha Sumatra na kuteketeza majengo yasiyopungua mia tano katika mji wa Padang.Mvua kubwa na idadi kubwa ya watu zinakwamisha juhudi za uokoaji.

Maafa ya Tsunami pia yamekikumba kisiwa cha Samoa ya Marekani katika eneo la Pasifik.

Katika kisiwa cha Sumatra wanajeshi na maafisa kutoka wizara ya afya wanaendelea na juhudi za kuwatafuta watu walionaswa chini ya mabaki ya nyumba na majengo yaliyoteketezwa.

Waliokufa ni pamoja na watoto wanane waliokuwa shuleni.Hatahivyo watoto wengine tisa walikutwa hai.

Wakati huo huo maafaisa wa serikali wamekiri kwamba pana uhaba wa vifaa, na hasa mashine kubwa. Lakini jeshi limesema ndege zenye shehena za mablanketi zimepelekewa. Wizara ya afya ya Indoneseia pia imesema imepeleka tani nane za dawa, tani nane za chakula cha watoto na wataalamu 200 wa tiba.

Rais Susilo Bambang Hudhoyono wa Indonesia ametoa mwito wa kupeleka misaada zaidi katika kisiwa cha Sumatra. Misaada pia imeanza kuwasili kutoka nje. Shirika la misaada, World Vision, limepeka wataalamu na limetenga kiasi cha dola milioni moja.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE

Mhariri. Miraji Othman