1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi laitikisa Taiwan

6 Februari 2016

Waokoaji katika mji wa kusini nchini Taiwan wa Tainan wamewapata watu 221 wakiwa hai na wengine watano wakiwa wamefariki kutoka katika jengo refu ambalo liliporomoka baada ya tetemeko la ardhi.

https://p.dw.com/p/1Hqfb
Erdbeben in Taiwan
Picha: picture-alliance/dpa/R. B. Tongo

Tetemeko hilo la ardhi lililokuwa katika kipino cha 6.4 lilitokea alfajiri leo Jumamosi(06.02.2016),na baadhi ya watu wakiwa bado wamenaswa katika kifusi. Wazima moto na wanajeshi walileta ngazi, winchi na vifaa vingine katika jebgo hilo ambalo liliporomoka na kuwa kifusi na kuwatoa watu kadhaa wakiwa hai.

Kituo cha kuchukua hatua za dharura kimeliambia shirika la habari la Associated Press kwamba watu watatu wameuwawa, ikiwa ni pamoja na mtoto mchanga wa miezi 10, mwanamke mwenye umri wa miaka 55 na mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 50.

Erdbeben in China, Helfer aus Taiwan Suche nach Überlebenden
Jengo lililoporomoka taiwanPicha: AP

Shirika rasmi la habari la Taiwan limesema mtoto huyo mchanga na mwanamume mmoja waliotolewa kutoka katika jengo hilo la ghorofa 17 lijulikanalo kama Wei Guan na kwamba watu hao walithibitishwa baadaye kwamba wamefariki.

Shirika hilo limesema watu 256 wanaaminika kuwa walikuwa wanaishi katika familia 92 katika jengo hilo.

Darzeni kadhaa zaidi za watu wameokolewa ama walioondolewa bila kupata madhara kutoka katika soko na jengo lenye ghorofa saba ambalo liliharibiwa vibaya, shirika hilo la habari limeripoti.

Jengo la benki pia liliharibika, lakini hakuna mtu aliyeripotiwa kuathirika, taarifa hiyo imesema.

Wengi wa watu wamejikuta katika hali hiyo wakati wakiwa wamelala wakati tetemeko lilipotokea saa za alfajiri.

Watu wengi zaidi huenda wamefukiwa katika kifusi

Tetemeko hilo lilitokea kiasi ya kilometa 36 kusini mashariki ya Yujing, na kushambulia kiasi ya kilometa 10 chini ya ardhi, kwa mujibu wa kituo cha uchunguzi wa miamba nchini Marekani.

Taiwan Erdbeben
Kituo cha uchunguzi wa tetemekoPicha: picture-alliance/dpa/D. Chang

Wakati alfajiri ilipofika , vituo vya televisheni nchini Taiwan vilionesha manusura wakitolewa kutoka katika kifusi hicho cha jengo lililoporomoka, ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja mzee wengine wakiwa wamefunikwa mablanketi.

Athari za tetemeko hilo zilihisiwa pia kote katika kisiwa hicho.

Waziri wa mambo ya ndani Chen Wei-jen amesema anahofia watu wengi zaidi bado wamo katika kifusi cha jengo hilo kuliko kawaida wakati wanafamilia huenda wamewasili ili kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya wiki ijayo.

Feuerwehrmänner bergen eine Verletzten nach einem Erdbeben nahe der taiwanesischen Hauptstadt Taipeh
Waokoaji wakiwaondoa watu kutoka majengo menginePicha: AP

Waziri mkuu wa nchi hiyo Chang San-cheng ametembelea eneo hilo la maafa , mama mmoja mtu mzima alilia , akisema mtoto wake wa kiume, mkwe wake wa kike na mjukuu bado wamenaswa katika kifusi cha jengo hilo katika ghorofa ya 15, limeeleza gazeti la Apple Daily.

Nchini Taiwan , watu 316 wamejeruhiwa, na wengine zaidi ya 60 wamepelekwa hospitali kutokana na majeraha, maafisa wamesema.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Isaac Gamba