1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thailand yaidhinisha katiba inayoungwa mkono na jeshi

7 Agosti 2016

Wananchi wa Thailand wameidhinisha katiba iliorasimiwa na jeshi katika kura ya maoni iliofanyika Jumapili (07.08.2016) na hiyo kufunguwa njia ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo mwaka 2017.

https://p.dw.com/p/1Jd5i
Picha: Reuters/C. Subprasom

 Wananchi wa Thailand wameidhinisha katiba iliorasimiwa na jeshi katika kura ya maoni iliofanyika Jumapili (07.08.2016) na hiyo kufunguwa njia ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo mwaka 2017.

Tume ya Uchaguzi wa Taifa imesema wakati asilimia 90 ya matokeo ya kura yakiwa tayari yamehesabiwa asilimia 61.5 ya wapiga kura wameiunga mkono katiba hiyo mpya wakati asilimia 38.4 wakiikataa.

Katiba hiyo iliyoandaliwa na baraza la kijeshi linaloiongoza nchi hiyo itaweka msingi wa serikali ya kiraia itakayouwa chini ya ushawishi wa kijeshi na kudhibitiwa na maafisa watakaoteuliwa badala ya kuchaguliwa.

Kura hiyo ya maoni kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikionekana kama mtihani kwa umashuhuri wa Waziri Mkuu Prayuth Chan-o-cha generali wa kijeshi aliyestaafu ambaye ameiingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 2014 na kuahidi kuitisha uchaguzi hapo mwaka 2017 baada ya kupitishwa kwa katiba hiyo mpya.

Takriban watu milioni 50 wamejiandikisha kupiga kura katika kura hiyo ya maoni ya Jumapili hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa wananchi hao wa Thailand kupiga kura tokea mapinduzi.

Ibara za mashaka katika katiba

Polisi akilinda usalama wakati wananchi wakipiga kura.
Polisi akilinda usalama wakati wananchi wakipiga kura.Picha: picture alliance/dpa/A. Wangni

Kamishna wa uchaguzi Somchai Srisutthiyakorn amesema idadi ya watu waliojitokeza ni aslimia 55 tu kinyume na iliyotarajiwa ya asilimia 70.

Kipindi cha kuelekea katika kura hiyo ya maoni kilikuwa kimegubikwa na shutuma za kimataifa kuhusiana na kupigwa marufuku kwa kampeni na takriban kutokea kesi 195 za watu kutiwa mbaroni.Wapinzani vikiwemo vyama vikuu vya kisiasa wamesema katiba hiyo itakomelea hatamu ya wanajeshi madarakani.Kwa upande wake jeshi linasema katiba hiyo mpya itadhibiti rushwa ya kisiasa na kuleta utengamano nchini humo.

Ibara zinazotiliwa mashaka makubwa kabisa ni zile zenye kutaka baraza la kijeshi liwachaguwe wabunge na kuziongezea madaraka mahakama za Thailand ambazo tayari zinashutumiwa kwa upendeleo wa kisiasa.Kifungu kengine kitafanya iwe rahisi kuanza mchakato wa kufunguwa mashtaka.

Mazingira ya hofu


Waziri Mkuu wa Thailand Prayuth Chan-Ocha.
Waziri Mkuu wa Thailand Prayuth Chan-Ocha.Picha: Getty Images/AFP/L. Suwandrumpha

Naibu mkurugenzi wa kanda hiyo wa Shirika la Haki za Binaadamu la Amnesty International Josef Benedict amesema mazingira kuelekea kura hii ya maoni yalikuwa ya kutisha.

Ameuliza iwapo watu hawawezi kutowa maoni kwa njia huru au kushiriki katika harakati za kisiasa bila ya hofu vipi wataweza kushiriki kwa njia ya tija katika kura hii ya maoni?

Kundi jengine la Wanasheria wa Haki za Binaadamu nchini Thailand limesema serikali imetumia sheria maalum ambayo inatamka kwa njia ya ubabaishaji marufuku kukosowa katiba hiyo.Jeshi liliwamimina maelfu ya makada kushajiisha watu wanaostahiki kupiga kura kushiriki kura hiyo ya maoni.

Madaraka yakipishana

Waziri mkuu wa zamani wa Thailaind Yingluck Shinawatra anayekabiliwa na mashtaka ya uzembe akionyesha kura yake.
Waziri mkuu wa zamani wa Thailaind Yingluck Shinawatra anayekabiliwa na mashtaka ya uzembe akionyesha kura yake.Picha: Getty Images/AFP/B. Sanchez-Trillo

Tokea mwaka 2006 madaraka yamekuwa yakipishana kati ya serikali zinazochaguliwa na wananchi zikiongozwa au kuwa na uhusiano na tajiri mkubwa anayeishi uhamishoni kwa hiari Thaksin Shinawatra au jeshi lililo tiifu kwa ufalme na washirika wake.

Hapo mwezi wa Mei mwaka 2014 serikali ya mwisho iliochaguliwa kidemokrasia nchini Thailand iliongozwa na dada wa Thaksin bibi Yungluck Shinawatra ilipinduliwa na jeshi kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya mitaani.

Hali mbaya ya afya ya Mfalme Bhumibol Adulyadej

ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 88 imefanya hali nchini humo kuzidi kuwa ngumu wakati vigogo wakikwaruzana kabla ya kuanzisha kipindi chochote kile cha mpito cha kisiasa.

Kufuatia ushindi huo wa kura ya maoni Waziri Mkuu Prayut Chan -o-cha ameshutumu ushawishi wa wageni nchini humo ambapo amesema kwa bahati mbaya kumekuwepo na baadhi ya uingiliaji kati usiofaa katika kipindi hiku kigumu nchini Thailand.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters/AP/AFP

Mhariri : Sylvia Mwehozi