1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May akabiliwa na upinzani katika mpango wa Brexit

12 Oktoba 2018

Theresa May amekuwa na wakati mgumu kupata makubaliano kuhusu mapendekezo ya mpango wake wa Brexit, ambayo yatakubalika na mawaziri wake, chama chake cha Conservatives na wabunge wa Ireland Kaskazini.

https://p.dw.com/p/36RvM
Birmingham Tory-Parteitag Rede Theresa May
Picha: Getty Images/AFP/B. Stansall

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May imesisitiza kuwa haitaiweka Uingereza mtegoni katika  suala la umoja  wa forodha usio  na kikomo  na  Umoja  wa Ulaya baada ya  kujitenga, mwezi M4echi mwaka ujao.  Hata hivyo msemaji wake amekataa kuthibitisha kwamba mpango wa kuuachia wazi mpaka wa ardhi na Ireland baada ya Uingereza kujiondoa mwezi Machi mwaka 2019 utakuwa wa muda mfupi.

Majadiliano mjini Brussels yamepiga hatua kabla ya kufanyika mkutano  wa kilele wa viongozi wa  Umoja wa Ulaya wiki ijayo, na May aliwaeleza baadhi ya wanachama katika baraza lake la mawaziri Alhamisi kuhusu jinsi anavyopanga kupata makubaliano. Uingereza imependekeza utaratibu wa forodha na Umoja wa Ulaya ili kuzuia ukaguzi wa kimwili kati ya Ireland Kaskazini na Ireland mwanachama wa Umoja wa Ulaya , hadi suala hilo litakaposuluhishwa na makubaliano ya biashara pana.

Mbunge mmoja mkosoaji katika chama cha Conservatives chake Theresa May, Andrea Jenkyns amekiomba chama hicho kumteua kiongozi mpya iwapo May  ataendelea na mpango huo wake wa Brexit, na kuutaja kuwa usaliti mkubwa wa kura ya Uingereza kutaka kujitenga na Muungano wa Ulaya. Wito wa Jenkins unafuatia upinzani wa baadhi ya mawaziri wakuu jana Alhamisi wakati May alipowaeleza mawaziri wake kwamba makubaliano ya kihistoria ya Brexit yanakaribia.

Großbritannien Theresa May in der Downing Street in London
Picha: picture-alliance/Photoshot

May anataka makubaliano ya biashara ya siku zijazo kuwa tayari ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2021. Chama cha Democratic Unionist kimetishia kuiangusha serikali iwapo mpango wa may utasabanisha kuwepo kwa vikwazo vya biashara kati ya Ireland Kaskazini na Uingereza bara.

Mwenyekiti wa halmashauri  kuu ya  Ulaya Jean Claude Junker amesema inawezekana  makubaliano ya Uingereza kujiondoa katika Umoja  wa Ulaya yakapatikana kati mkutano wa viongozi wakuu  wa Umoja  wa Ulaya  wiki ijayo mjini Brussels, na mwengine mwezi Novemba, lakini suala la  Ireland linabakia kuwa  la kutatanisha.

Mwandishi: Sophia Chinyezi

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman