1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May azidi kuonya kuhusu Brexit kabla ya kura bungeni

Caro Robi
10 Desemba 2018

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ameonya kuwa iwapo bunge litapinga makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit basi huenda nchi hiyo ikashindwa kuondoka kutoka umoja huo.

https://p.dw.com/p/39miD
Großbritannien | Theresa May im House of Commons
Picha: picture-alliance/dpa/empics/Pa Wire

Kauli hiyo ya May inakuja huku serikali yake ikihofia kuwa itapata pigo kubwa katika kura inayotarajiwa kesho Jumanne bungeni kuidhinisha au kupinga makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita. 

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinaripoti kuwa May anashinikizwa na baraza lake la mawaziri kuchelewesha kura hiyo na kuelekea Brussels kufanya majadiliano zaidi na viongozi wa Umoja wa Ulaya ili kufikia makubaliano yatakayoridhiwa na wabunge wengi kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya unaotarajiwa Alhamisi na Ijumaa wiki hii.

Mbivu na mbichi kuhusu Brexit kujulikana Jumanne

Lakini waziri wa Uingereza anayeshughulikia Brexit Stephen Barclay amesema kura hiyo itafanyika kesho kama ilivyopangwa.

Parteitag 2018 der britischen Labour Party in Liverpool
Kiongozi wa Upinzani wa Uingereza Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/ZumaPress/R. Pinney

May amesisitiza kuwa kupinga mpango wake kuhusu Brexit uliofikiwa na pande zote mbili baada ya mazungumzo ya karibu miaka miwili, kutaitumbukiza Uingereza katika mashaka makubwa, huku ikiwa imesalia chini ya miezi minne kabla ya nchi hiyo kuondoka rasmi kutoka Umoja wa Ulaya mwezi Machi mwakani.

Waziri huyo mkuu wa Uingereza ameongeza kusema wana kiongozi wa upinzani ambaye hafikirii lolote isipokuwa kuitishwa kwa uchaguzi mkuu na kusisitiza kuwa anaamini kutakuwa na hatari iwapo Jeremy Corbyn atashikilia madaraka, jambo ambalo Waingereza hawapaswi kuliruhusu.

Chama cha Corbyn cha Labour kinatumai kuwa mpango wa May kuhusu Brexit utashindwa kesho bungeni na kuchochea uchaguzi wa mapema utakaokipa chama hicho ushindi na kuingia madarakani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010.

Hayo yanakuja huku mahakama ya sheria ya Umoja wa Ulaya ECJ ikitarajiwa kutoa uamuzi leo kuhusu iwapo Uingereza inaweza kubatilisha mpango wake wa kuondoka katika Umoja wa Ulaya, kesi inayofuatiliwa kwa karibu na wale wanaotaka kura ya pili ya maoni kuitishwa kaumua mustakabali wa taifa hilo ambalo limekuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya kwa miaka 46.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga