1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tillerson aanza ziara ya bara la Afrika

Sekione Kitojo
8 Machi 2018

Ziara ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson katika bara la Afrika inajumuisha kurekebisha baadhi ya mambo ya  kidiplomasia baada ya rais Trump kutoa matamshi yenye utata kuhusu baadhi ya nchi za Afrika.

https://p.dw.com/p/2tyEm
Äthiopien Rex Tillerson
Picha: Reuters/J. Ernst

Rais wa  halmashauri  ya  Umoja  wa Afrika  Moussa  Faki  amepuuzia  tukio  hilo  na  kusema  ni  "mambo yaliyopita". Tillerson hata  hivyo  amezitahadharisha  nchi  za  Afrika kutotupa uhuru wao kwa  kukubali  mikopo kutoka  China.

Mapema mwaka  huu , rais  wa  Marekani  Donald Trump alisababisha  hasira  katika  bara  hilo  baada  ya  kuripotiwa akisema  kwamba  baadhi  ya  nchi  za  Afrika  ni  kama zimo  katika shimo  lenye  uvundo, na  kusababisha  mataifa  kadhaa  kuwaita mabalozi wa  marekani  katika  nchi  zao  kupta  ufafanuzi na  kudai kuombwa  msamaha.

Äthiopien Moussa Faki Kommissionsvorsitzender Afrikanische Union (AU)
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Kumekuwa  na  uvumi  kwamba  Rex Tillerson  anaweza  kukabiliwa na  uhasama  katika  ziara  yake  ya  Afrika  kutokana  na  matamshi hayo, lakini  mwenyekiti  wa  halmashauri  ya  Umoja  wa  Afrika Moussa Faki  amepuuzia  maswali  kuhusu  suala  hilo katika mkutano  na  waandishi  habari akiwa  pamoja  na  waziri  Tillerson mjini  Addis Ababa leo Alhamis.

"Naamini  kwamba  tukio  hilo  kuhusiana  na  matamshi  ya  rais Trump  kuhusu  Afrika  limepita. Naamini  kwamba  ziara  hii  leo ya waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani Tillerson ni uthibitisho wa  uhusiano  baina  ya  Afrika  na  Marekani."

Tillerson atangaza  misaada  kwa Afrika

Ziara  hiyo  ya  Afrika , ambayo  pia  inajumuisha  Chad, Djibouti, Kenya na  Nigeria  ni  ya  kwanza  kufanywa  na  Tillerson  tangu alipokuwa  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani, na alitangaza  zaidi  ya  dola  nusu bilioni  za  misaada  kabla  ya kuanza  ziara  hiyo. Tillerson  amesema  Marekani  inatoa  msaada wa  kiutu , kupambana  na  njaa  na  ukame  pamoja  na  hali  ya kutokuwa  na  uhakika  wa  chakula.

Äthiopien Rex Tillerson und Moussa Faki Kommissionsvorsitzender Afrikanische Union (AU)
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson akilakiwa na rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki mjini Addis AbabaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Akiwa  katika  mji  mkuu  wa  Ethiopia  leo, Tillerson amezungumzia kuhusu  hali  ya  China  kusambaa  katika  bara  hilo, akizitahadharisha  nchi  hizo kutotupa uhuru  wao.

"Tuna shuhudia  kauli  mbiu  ambayo  China  inaifuata. Hawaleti uwezo  wa  ujenzi  wa  nafasi  za  kazi, hawaleti  mipango  halisi  ya mafunzo ambayo  itawawezesha  Waafrika  kushiriki zaidi  katika maisha  ya  baadaye, na  mara  nyingi utaratibu  wa  utoaji  wa mikopo  uko katika  njia  kwamba  nchi , inapopata  matatizo  kifedha, inapoteza  uwezo  wa  kudhibiti  miundo  mbinu  yake ama  maliasili zake  kutokana  na  kushindwa  kulipa."

Tillerson  amesema  Marekani  haijaribu  kuondoa uwekezaji  wa China  kutoka  bara  la  Afrika , lakini  amesema , "ni  muhimu kwa nchi  za  Afrika  kutafakari  kwa  uangalifu  masharti ya  uwekezaji huo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman