1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu tano za mwisho kufuzu katika duru ya 16

8 Desemba 2014

Nafasi tano za duru ya mtoano zinatarajiwa kushindaniwa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, na mashabiki wanatarajia kushuhudia msisimko wa dakika za mwisho mwisho katika duru ya mwisho ya makundi.

https://p.dw.com/p/1E0wv
Champions League Manchester City vs. AS Roma 30.9.2014
Picha: Reuters

Timu kumi na moja tayari zimefuzu katika 16 za mwisho. Na timu hizo ni Real Madrid, Atletico Madrid, Barcelona, Bayer Leverkusen, Borussia Dortmund, Bayern Munich, Arsenal, Chelsea, Paris St Germain, Porto na Shakhtar Donetsk.

Timu mbili za Italia, Juventus na Roma na timu mbili za Uingereza Manchester City na Liverpool ni miongoni mwa timu 11 zinazowania nafasi ya kufuzu katika duru ya mchujo, na mchuano wa Roma nyumbani Jumatano usiku nyumbani dhidi ya Manchester Coty utaangaziwa macho. Roma, City na CSKA Moscow zote zina points tano katika Kundi E, lakini mfumo wa kutathmini ni nani bora kuliko mwingine kutokana na idadi ya magoli, unaegemea upande wa Roma ambao wanastahili kushinda ili kufuzu, au watoke sare kama CSKA watashindwa kuwapiku viongozi Bayern.

Champions League Basel - Liverpool 01.10.2014
Liverpool inalenga kujikatikia tikiti katika mechi ambayo lazima washinde dhidi ya BaselPicha: Reuters/A. Wiegmann

Nao mabingwa wa England City wanastahili kushinda na kuomba kuwa CSKA haitaishinda Bayern, nao Warusi hao wataweza kufuzu kama watashinda na kisha na Roma ikose kuipiku City.

Hali ni rahisi katika Kundi B ambako Liverpool lazima wawashinde Basel ili kujiunga na Real Madrid katika awamu ya mchujo, wakati nayo klabu hiyo ya Uswisi ikihitaji sare ya aina yoyote ili kuwatema nje mabingwa hao wa Ulaya mara tano.

Katika Kundi C, Monaco inahitaji sare nyumbani dhidi ya Zenit St Petersburg ili kujiunga na Bayer Leverkusen, wakati Warusi hao wakistahili kushinda. Kama mechi hiyo itakamilika kwa sare ya kutofungana goli, Monaco itafuzu licha ya kuwa imefunga tu magoli mawili pekee katika mechi sita.

Mabingwa wa Serie A Juventus wanahitaji point moja nyumbani dhidi ya Atletico Madrid kesho ili kuepuka marudio ya msimu uliopita walipobanduliwa nje ya awamu ya makundi. Kama warashindwa na kisha Olympiakos wawazabe Malmo nyumbani, basi mabingwa hao wa Ugiriki watafuzu.

Tikiti ya mwisho kushindaniwa ni katika Kundi G, ambapo Sporting Lisbon itahitaji tu sare ugenini dhidi ya Chelsea, kama mahasimu wao wa Ujerumani Schalke 04 watashindwa kuwashinda Maribor. Schalke lazima wawashinde Maribor na kutumai kuwa Sporting itachapwa na Chelsea. Katika kundi F, Barcelona lazima wawashinde Paris St Germain kama watataka kumaliza kama viongozi wa kundi hilo. Droo ya mechi za duru ya 16 bora itafanyika Desemba 15 ambako washindi wa makundi yote manane watapangwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman