1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za Tanzania zafurushwa mapema Kagame Cup

Aboubakary Jumaa Liongo6 Julai 2009

Ni Jumatatu nyingine ambapo tunakutana katika ukurasa huu wa michezo kutoka idhaa ya kiswahili ya DW Bonn.

https://p.dw.com/p/IiCe

Naam tuanze basi na patashika ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati Kagame Cup huko Sudan, ambapo timu za Tanzania, Prison na Miembeni zimefungashwa virago mapema, huku Mathare ya Kenya ikiwa ni miongoni mwa zile zilizofuzu.


Michuano hiyo safari hii imewashirikisha mabingwa wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, TP Mazembe kama timu alikwa.


Timu hiyo ya Tp Mazembe imeonesha kabumbu la kuvutia kiasi kwamba wengi wanaamini kuwa watatwaa ubingwa huo.



Huko huko Barani Afrika,hapo jana , Timu ya taifa ya soka ya Misri ikicheza nyumbani mjini Cairo, iliishindilia Rwanda mabao 3-0 katika mechi za kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la duniani mwaka ujayo.


Mabao mawili ya Mohamed Aboutrika na moja la Hosni Abd Rabou yamewanyanyua mabingwa hao wa Afrika hadi katika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi C wakiwa na pointi 4 sawa na Zambia.Algeria ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 7.


Barani Ulaya, Nahodha wa zamani wa Ujerumani Franz Beckenbauer amesema kuwa anaamini bara hili ndilo linalostahiki kuandaa fainali za kabumbu za dunia za mwaka 2018, ambapo hata hivyo hakuinyooshea kidole nchi yoyote, lakini hakusita kusema Uingereza inaweza jukumu hilo.


Akizungumza na gazeti moja la Australia, Beckenbauer amesema angependa kuona fainali hizo za mwaka 2018 zikifanyika Ulaya.


Beckenbauer ni mmoja kati ya wajumbe 24 wa kamati kuu ya shirikisho la kandanda duniani FIFA watakaokutana Decemba mwakani kuamua ni nchi gani zitakuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2018 na 2022.


Huko Mashariki ya Kati timu ya taifa ya kandanda ya Palestina Ijumaa ijayo inaekelea Iraq kupambana na timu ya taifa ya nchi hiyo, kabla ya kuelekea China kwa ziara nyingine.


Kiongozi wa Shirikisho la soka la Palestina Jibril Rajab amesema timu ya taifa ya Palestina itapambana na ile ya Iraq katika mji wa Arbil, ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuondoka kwa majeshi ya Marekani huko Iraq.


Baadaye timu hiyo itaelekea China kwa mechi kadhaa za kirafiki.


Hapa Ujerumani, kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Ze Roberto ametangaza kujiunga na Hamburg inayoshiriki katika Bundesliga kwa mkataba wa miaka miwili.


Ze Roberto alikuwa ikiichezea Bayern Munich, ambapo akiwa na timu hiyo amefanikiwa kutwaa mataji manne ya ligi ya Bundesliga na manne ya vikombe vingine hapa Ujerumani.


Kocha wa Hamburg Bruno Labbadia amesema ni furaha kwao kumpata mchezaji mwenye uwezo na uzoefu kama Ze Roberto.


Mwandishi:A.Liongo/RTRE /AFP

Mhariri:Abdul-Rahman