1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za Ulaya zinaweza kufanikiwa Brazil?

22 Mei 2014

Katika majaribio saba, hakuna nchi ya Ulaya iliyowahi kushinda Kombe la Dunia katika nchi za Amerika, lakini takwimu hiyo itakumbwa na kitisho kikubwa wakati wa kinyang’anyiro cha mwaka huu nchini Brazil.

https://p.dw.com/p/1C4Lc
Fußball WM Finale Spanien Niederlande Weltmeisterschaft Siegerehrung
Picha: dapd

Wakati timu, tangu jadi zikijitahidi sana kutamba katika mabara ya kigeni, ongezeko la utandawazi michezoni na kuimarishwa teknolojia vina maana kuwa kucheza katika ardhi ya nyumbani hakuna tena faida kama ilivyowahi kuwa wakati mmoja.

Kwa mtazamo halisi wa kispoti, timu 13 kutoka shirikisho la Soka barani Ulaya – UEFA, ambazo zinaelekea Brazil zitafanya hivyo katika wakati ambapo bara ulaya linatawala.

Tatu kati ya timu nne zilizofika katika nusu fainali ya dimba la Kombe la Dunia mwaka wa 2010 zilikuwa za Ulaya na sita kati ya Vikombe saba vya Klabu bora Ulimwenguni vimenyakuliwa na timu za Ulaya, isipokuwa tu ushindi wa klabu ya Brazil, Corinthians, dhidi ya Chelsea katika mwaka wa 2012.

Wakati huo huo, ijapokuwa nyota ya Argentina Lionel Messi ametawala tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka ulimwenguni – FIFA Ballon d‘Or katika miaka ya karibuni, mara ya mwisho ambayo mchezaji mwingine wa Amerika ya Kusini alipanda jukwaani ilikuwa wakati Kaka alipotunukiwa tuzo hiyo mwaka wa 2007.

Lionel Messi ameichezea Barcelona tangu akiwa na umri wa miaka 13
Lionel Messi ameichezea Barcelona tangu alipohamia uhispania akiwa na umri wa miaka 13Picha: Getty Images

Messi pia ni mfano mzuri wa mchezaji kutoka Amerika ya Kusini ambaye amecheza miaka mingi barani Ulaya kuliko bara ambalo alizaliwa.

Jinsi kocha wa England Roy Hodgson alivyosema mapema mwaka huu, uhamisho mkubwa wa wachezaji wa Amerika ya Kusini barani Ulaya una maana kuwa huenda wasijihisi sana kuwa nyumbani wakati wakicheza nchini Brazil kuliko wenzao wa kutoka Ulaya.

Usafiri pia ni sababu nyingine kuu ambayo siyo ya kubabaisha sasa kuliko wakati ilivyokuwa kwa wachezaji wa Ulaya waliosafiri kucheza mashindano ya mwanzo ya Kombe la Dunia yaliyoandaliwa katika Amerika ya Kusini – nchini Uruguay mwaka wa 1930, Brazil 1950 na Chile 1962.

Wakati timu nne za Ulaya zilizoshiriki katika dimba la kwanza la Kombe la Dunia nchini Uruguay walivuka bahari ya Atlantic kwa kutumia mashua, wengi wa wachezaji watakaocheza nchini Brazil mwaka huu watawasili kwa njia ya kifahari ndani ya ndege.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir