1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu zote za nyumbani zashindwa kutamba Bundesliga

30 Septemba 2019

Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga ilishuhudia mechi za mzunguko wa sita kuchezwa mnamo mwishoni mwa wiki ambapo kuliwekwa rekodi ya timu nane za ugenini kupata ushindi katika wikendi moja.

https://p.dw.com/p/3QUMr
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Werder Bremen
Picha: Reuters/L. Kuegeler

Jumapili Freiburg ndio waliokamilisha orodha hiyo ya timu nane kushinda ugenini walipowalaza Fortuna Düsseldorf magoli mawili kwa moja.

Hapo Jumapili pia FC Köln waliokuwa nyumbani walinyeshewa nne bila na Hertha BSC Berlin.

Matokeo haya yanamaanisha kwamba hakukuwa na timu ya nyumbani iliyotoa ushindi kwenye mechi za wikendi kwa kuwa Borussia Dortmund waliokuwa kwao walilazimishwa sare ya mbilimbili na Werder Bremen.

Hii ni mara ya saba katika historia ya Bundesliga ambapo timu zote za nyumbani zimeshindwa kutoa ushindi, mara ya mwisho kutokea ilikuwa mwaka 2015.

Bayern Munich walikuwa ugenini na walikuwa na kazi ngumu dhidi ya Paderborn ingawa walipata ushindi wa magoli matatu kwa mawili huku waliokuwa vinara RB Leipzig wakilazwa tatu moja nyumbani kwao walipokuwa wakivaana na Schalke 04.