1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Touadera aongoza matokeo ya awali Jamhuri ya Afrika ya Kati

4 Januari 2016

Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadera, anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa jana, ambapo amepata asilimia 23 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/1HXYz
Afrika Wahlen in Zentralafrika
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Maafisa wa uchaguzi wamesema Touadera mwenye umri wa miaka 58, anaongoza katika matokeo hayo ya awali baada ya kupata kura 120,000, ambazo ni robo ya kura zilizohesabiwa hadi sasa.

Touadera profesa wa hesabu na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wa utawala wa muda mrefu wa Francois Bozize kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, ameshiriki katika uchaguzi huo kama mgombea binafsi, katika kinyang'anyiro hicho kilichokuwa na wagombea 30.

Katibu wa Tume ya Uchaguzi, Julius Ngouade Baba amesema nafasi ya pili inashikiliwa pia na Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Anicet Georges Dologuele ambaye amepata zaidi ya kura 68,500 zilizohesabiwa hadi sasa.

Askofu Mkuu wa Bangui, Dieudonne Nzapalaingaa, akiwabariki watu kabla ya kupiga kura
Askofu Mkuu wa Bangui, Dieudonne Nzapalaingaa, akiwabariki watu kabla ya kupiga kuraPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Disire Kolingba, mtoto wa rais wa zamani, anashika nafasi ya tatu baada ya kupata kura 40,000, huku nafasi ya nne ikichukuliwa na Jean-Serge Bokassa, mtoto wa Jean-Bedel Bokassa aliyejitangazia ufalme wa nchi hiyo na kutawala kuanzia mwaka 1966 hadi 1979, ambaye amepata kura 34,000.

Waziri Mkuu wa zamani, Martin Ziguele, ambaye alionekana kama mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kushinda na kipenzi cha Ufaransa, ameshika nafasi ya tano baada ya kupata kura 28,000.

Wabunge pia wachaguliwa

Karibu watu milioni mbili wenye uwezo wa kupiga kura katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, pia wamewachagua wanasiasa 1,800 wanaogombea viti 105 vya bunge la nchi hiyo. Taarifa zinaelezea Tume ya Uchaguzi inaweza kutangaza matokeo rasmi katika kipindi cha hadi siku 15. Duru ya pili ya uchaguzi wa rais imepangwa kufanyika Januari 31, mwaka huu.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo-MINUSCA, kimeuelezea uchaguzi huo mkuu uliofanyika Jumatano iliyopita, kama uliofanikiwa, licha ya kuwepo mapungufu kadhaa yaliyosababishwa na kucheleweshwa kwa zoezi la kupiga kura kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Akizungumza baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Mkuu wa kikosi cha MINUSCA, Parfait Onanga-Anyanga alisema wameridhishwa na uchaguzi huo. Naye kamanda wa kikosi cha jeshi cha MINUSCA, Balla Keita amesema wamefanya muujiza katika nchi yenye vita.

Wanajeshi wa MINUSCA
Wanajeshi wa MINUSCAPicha: P. Pabandji/AFP/Getty Images

Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye waumini wengi wa Kikristo, ilitumbukia kwenye vita baada ya kundi la waasi la Seleka lenye Waislamu wengi, kumuondoa madarakani Rais Francois Bozize, mwezi Machi, 2013 katika mapinduzi yaliyouingiza madarakani utawala wa Kiislamu wa Michel Djotodia.

Bozize na Djotodia wote walipigwa marufuku kugombea katika uchaguzi huo mkuu. Kwa sasa viongozi hao wa zamani wanaishi uhamishoni na wanakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa kutokana na ghasia za nchini humo zilizosababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine kuyakimbia makaazi yao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef