1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump asema ataiondoa Rwanda kwenye mkataba wa AGOA.

17 Aprili 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amelifahamisha bunge kuwa katika kipindi cha siku 60 ataisimamisha Rwanda kwenye mkataba wa kuziruhusu nchi za Afrika kuuza bidhaa katika soko la Marekani bila kutozwa ushuru.

https://p.dw.com/p/2wBob
Nairobi Gikomba Second-Hand Markt
Picha: picture-alliance/dpa/D. Irungu

 

Mkataba huo unaojulikana kama AGOA,umepokelewa kwa mchanganyiko wa hisia.

Chini ya mkataba wa AGOA, bidhaa kutoka mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara huingia katika soko la Marekani bila ya kutozwa ushuru. Lengo la mkataba huo ni kusaidia nakushajiisha  biashara na ustawi kupitia mauzo ya nje.

Fundi mmoja wa magari nchini Rwanda aliyeloa jasho anatafuta suruali ya jeans moja baada ya nyingine kwenye robota la nguo kuukuu (mitumba) bila ya kufahamu vita vya kibiashara alivyovianzisha rais wa Marekani Donal Trump.

Nguo kuukuu  yaani mitumba mbazo zimetumiwa na Wamarekani na kuuzwa kwa mataifa ya Afrika ni biashara yenye kima cha mamilioni ya fedha, ila imelaumiwa kwa kusambaratisha viwanda vya nguo katika mataifa mengi.

Rwanda yaongeza ushuru wa mitumba

Sasa Rwanda imechukua hatua ya kuongeza ushuru kwa nguo hizo kinyume na shinikizo za Marekani. Kwa upande wake Marekani imesema kuwa itasimamisha hatua yake ya kutotoza Rwanda ushuru kwa bidhaa zake zinazouzwa Marekani kwenye mkataba unaoyaruhusu mataifa ya Afrika kuuza bidhaa zake nchini Marekani bila ya kutozwa ushuru-AGOA.

USA - Trump ordnet Militärschlag auf Syrien an
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/AP/S. Walsh

Hatua ya rais Donald Trump haijachukuliwa vizuri na Rwanda, taifa dogo ambalo lililoko Afrika Mashariki linajorabu kuimarika baada ya makovu ya vita vya kimbari vilivyofanyika miaka 24 iliyopita.

Hatua sawa na hizo za Marekani huenda zikatekelezwa dhidi ya mataifa jirani; Uganda na Tanzania zimeapa kuongeza ushuru wao na kupiga marufuku uagizaji wa nguo kuukuu ifikapo mwaka 2019.

Hatua dhidi ya Rwanda inajiri majuma machache ambapo rais Paul Kagame alikutana na Trump katika Kongamano la Kiuchumi Ulimwenguni na kumuita Trump rafiki, kwa nia ya kumtuliza baada ya Trump kutumia matamshi ya matusi kuhusu bara la Afrika.

Kwa sasa Kagame ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambapo baada ya matamshi ya Trump viongozi wa mataifa kadhaa waliandika barua ya pamoja kuhusu Trump lakini wakaamuua kutoitangaza.

Hatua ya Marekani inaibua mseto wa hisia kutoka barani Afrika, huku baadhi wakikosoa Trump tena na wengine wakiitetea biashara ya nguo za mitumba zilizo maarufu na za bei nafuu.

Dismas Nkurunga ambaye ni muuzaji wa nguo hizo katika mji mkuu wa Kigali anasema Marekani inalemaza juhudi za Rwanda za kuimarisha viwanda vyake vya nguo.  

Rwanda yasema inalenga kuboresha viwanda vyake

Waziri wa nchi anayehusika na  masuala ya nchi za nje Olivier Nduhungirehe, anasema, "malengo ya Rwanda ni kuwa na viwanda vingi vya kutengeza nguo." Anongeza kusema, "hatua hiyo pia ni kuipa nafasi Rwanda kuwa na heshima wanayostahili sio kuvaa nguo za mitumba ambazo zimetumika na watu wengine."

Afrika Kenia Altkleider
Biashara ya mitumba Afrika Picha: AP

Lakini katika soko kubwa la Owino katika mji mkuu wa Kampala nchini Uganda, biashara ya nguo za mitumba inashamiri huku wauzaji wakishikilia nguo hizo kuwashawishi wanunuzi kwa bei nafuu.

John Ekure, ambaye ni fundi wa magari anasema, "kile ambacho anataka ni nguo zenye bei nafuu huku akipekua pekua suruali kadhaa."

Huku baadhi ya serikali za Afrika zikiwa na wasiwasi kuhusu nguo nyingi zinaoagizwa na kurundikwa wengine wanahofu iwapo viwanda vya afrika vitakidhi ubora wa nguo hizo.

Uhaba wa mitumba washuhudiwa Rwanda

Rwanda imekuwa ikiunga mkono wawekezaji wa China kujenga viwanda vya nguo ikitumai kuwa taifa hilo hatimaye litaweza kutengeza nguo zake na kubuni nafasi laki tatu na nusu za kazi ifikapo mwaka 2025.

Nchini Uganda, wafanyibiashara na wanunuzi wanasema kuwa wanatarajia kuwa serikali haitachukua hatua ambayo Rwanda imechukua ya kuongeza kiwango cha ushuru kwa nguo zilizotumika.

Mfanyibishara mmoja alisema kuwa idadi ya Warwanda wanaokuja Uganda kutafuta nguo inazidi kuongezeka kwa kuwa bidhaa hizo hazipatikani tena nchini mwao.

Ramathan Ggoobi, mchumi katika chuo kikuu cha Makerere kilichoko Ugunda anasema, "hatua ya Rwanda itasababisha madhara mengi zaidi ya manufaa. Kwani hakuna viwanda kwa sasa kwa hivyo unalinda mzalishaji ambaye hana bidhaa za kutosha."

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman