1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aionya Korea Kaskazini kwa mara nyingine

Isaac Gamba
9 Agosti 2017

Rais Donald Trump wa Marekani ameionya  Korea Kaskazini akiahidi kuwa iwapo nchi hiyo itaendelea  na vitendo vyake vya uchokozi basi itakabiliwa na hatua kali ambazo dunia haijawahi kuzishuhudia.

https://p.dw.com/p/2hvN5
Donald Trump
Picha: Picture-Alliance/AP Photo/E. Vucci

 Rais Trump ametoa onyo hilo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Bedminster New Jersey ambako yuko mapumzikoni. 

Trump hakutoa maelezo zaidi  mnamo wakati vita vya maneno  kati ya Marekani na Korea Kaskazini  vikizidi kushika kasi katika siku za hivi karibuni vinavyosababishwa na  hatua zinazochukuliwa na Korea Kaskazini kuhusiana  na mipango yake ya silaha za nyukilia , majaribio ya makombora ya masafa marefu pamoja na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo.

Juhudi za Marekani katika siku za hivi karibuni  zimekuwa zikilenga kuongeza mbinyo kwa Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kukabiliwa na vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa ikiwa ni sehemu ya  hatua za kutaka nchi hiyo iachane na mipango yake ya silaha za nyukilia.

Marekani pia tayari  imeonyesha uwezo wake kijeshi kwa kudungua kombora  na imefanya mazoezi ya pamoja  ya kijeshi na Korea Kusini katika wiki za hivi karibuni.

Mapema kupitia katika ukurasa wa twitter rais Donald Trump alisema " baada ya kushindwa miaka mingi hatimaye sasa mataifa yanaungana pamoja ili kutafuta njia ya kukabiliana na hatari inayoweza kusababishwa na Korea Kaskazini tunapaswa kuwa thabiti"

Siku moja kabla Korea Kaskazini ilisema haina mpango wa kutumia silaha za nyukilia dhidi ya yeyote isipokuwa Marekani na kuongeza kuwa katika mazingira yoyote haitakuwa tayari kujadili juu ya mpango wake unaohusiana na silaha za nyukilia.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Yong Ho ameishutumu Marekani kwa kusababisha hali ambayo amesema inaonekana kuilazimisha Korea Kaskazini ichukue hatua za kujilinda na kuongeza  kutokana na hilo mgogoro katika rasi ya Korea utazidi kukua.

Uchambuzi wa Marekani kuhusiana na masuala ya kijeshi uliochapishwa jana katika gazeti la Washington Post umeonesha kuwa Korea Kaskazini tayari imepiga hatua katika kumiliki sampuli ya vichwa vya makombora ya nyukilia na hii  inafuatia tathimini iliyofanywa awali inayoonyesha kuwa mipango ya utawala wa nchi hiyo kuhusiana na silaha za nyukilia iko katika hatua ya juu zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo kabla.

Japan nayo yaonya juu ya uwezo wa silaha za nyukilia wa Korea Kaskazini

Japan Shinzo Abe
Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo AbePicha: Getty Images/AFP/T. Yamanaka

Japan katika tathimini yake nayo pia imedokeza  juu ya uwezekano Korea Kaskazini kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyukilia na kuonya kuwa hatua hiyo itazidisha vitendo vyake vya uchokozi.

Hatua zinazochukuliwa na Korea Kaskazini za kujiimarisha katika nyanja inayohusiana na silaha za nyukilia  pamoja na makombora ya masafa marefu zinaashiria awamu nyingine mpya ya vitisho kutokana na nchi hiyo kufyatua makombora  ya masafa marefu  zaidi ya 20 katika kipindi cha mwaka jana pekee. Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa waraka wa  kila mwaka wa Japan  unaohusiana na masuala ya ulinzi.

Mwezi uliopita kwa mara ya kwanza  Korea Kaskazini ilifyatua kombora linalotoka bara moja kwenda jingine na kufuatiwa na jaribio lingine la pili wiki kadhaa baadaye.

Wakati huohuo mnamo wakati mvutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini ukizidi kukuwa  meya wa mji wa Nagasaki nchini Japan Tomihisa Taue  hii leo  katika hafla ya kumbukumbu ya miaka 72 tangu Marekani iliposhambulia mji huo kwa bomu la atomiki amesema hofu ya shambulizi lingine la bomu la nyukilia inazidi kuongezeka.

Meya huyo ametoa mwito kwa mataifa yenye nguvu za nyukilia kuzuia silaha hizo za nyukilia na kuikosoa serikali ya Japan kwa kushindwa kushiriki katika juhudi za kidunia  za kupiga marufuku silaha za nyukilia.

Mwandishi: Isaac Gamba/ dpae/ape

Mhariri: Josephat Charo