1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akanusha Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani

Isaac Gamba
4 Agosti 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa madai ya kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 ni uzushi mtupu mnamo wakati vyombo vya habari nchini humo vikiripoti kuwa tume maalumu inachunguza tuhuma hizo.

https://p.dw.com/p/2hgQ6
USA Präsident Donald Trump
Picha: Reuters/J. Roberts

Trump ameyasema hayo katika mkutano uliofanyika Huntington Virginia na kusisitiza kuwa madai hayo ni ya uzushi na ni kisingizio kutokana na wapinzani wake kutokuwa na hoja ya kusema au malengo baada ya kushindwa uchaguzi.

Trump ameongeza kuwa Watu wengi wanajua fika kuwa hakukuwa na warusi katika kampeni zao na kuwa  hawakushinda kwasababu ya Urusi ila walishinda kwa sababu ya wapiga kura kuwachagua.

Vyombo vya habari  vimeripoti kuwa kiongozi wa tume maalumu ya uchunguzi Robert Mueller ameunda jopo la majaji  kuchunguza sakata hilo njia ambayo waendesha mashitaka hupata nyaraka au hulazimisha mashahidi kutoa ushahidi kuhusaiana na kesi muhimu za kijinai.

Baadhi ya majaji wanaofuatilia  tuhuma hizo katika wiki za hivi karibuni walikuwa wakitafuta nyaraka zinazohusiana na masuala ya kibiashara yanayomhusu Michael Flynn , aliyekuwa mshauri wa kitaifa katika masuala ya usalama wa Rais Trump. Hiyo ni kwa mujibu wa gazeti la New York Times katika taarifa yake likiwanukuu wanasheria wanaofuatilia tuhuma hizo.

USA Sonderermittler Robert Mueller
Robert Mueller, Kiongozi Mkuu wa tume inayochunguza tuhuma dhidi ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani. Picha: picture-alliance/Consolidated News Photos/Ron Sachs - CNP/R. Sachs

Jarida la Wall Street mapema liliripoti kuwa   kiongozi  maalumu anayechunguza madai ya Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka jana alikuwa tayari ameunda jopo hilo la majaji kufuatilia tuhuma hizo.  Jopo la majaji hujumuisha raia wa kawaida  ambao wanaweza kuamua kutoa hati ya kuitwa kuhojiwa  na mashauri ya aina hiyo huendeshwa kwa faragha.

Michael Flyn  aliyejiuzulu  mwezi Februari mwaka huu baada ya kukiri kutoa taarifa zisizojitosheleza kuhusiana na mawasialiano kati yake na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak  naye pia ameitwa na jopo  la majaji  la Virginia  pamoja, kamati ya baraza la seneti  na ile ya baraza la wawakilishi.

 Shirika la habari la CNN limeripoti kuwa jopo lingine la majaji lililoundwa kufuatilia sakata hilo liliitisha  nyaraka kutoka kwa watu waliohusika katika vikao vilivyomkutanisha mtoto wa kiume wa Rais Trump, Trump Juniour na mwanasheria  wa Urusi. 

Mwanasheria wa Trump amesema hakuwa na taarifa kuhusiana na jopo la majaji lililoundwa kufuatilia kadhia hiyo kama ilivyoripotiwa na jarida la Wall Street lakini akasema ikulu ya White House itaendelea kushirikiana na Mueller kiongozi mkuu wa uchunguzi  huo.

Kamati ya baraza la seneti pamoja na ile ya baraza la wawakilishi pamoja na tume huru wanachunguza iwapo kulikuwa na makubaliano kati ya wajumbe wa timu ya kampeni ya Trump na Urusi katika kujaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka jana.

Mashirika ya ujasusi ya Marekani yanasisitiza kuwa Urusi ilifanya udukuzi wa barua pepe za  chama cha Democratic kwa madhumuni ya kumfanya Hillary Clinton mgombea wa chama cha Democratic asishinde uchaguzi huo.

Waendesha mashitaka wameonyesha wasiwasi wao kuwa Rais Trump anaweza akaingilia uchunguzi huo unaoongozwa na Mueller au atafute njia za kumfuta kazi.

 Hata hivyo maseneta wawili hii leo wamewasilisha muswada ambao utafanya iwe vigumu kwa Rais kufanya hivyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga