1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amfuta kazi Rex Tillerson

Yusra Buwayhid
13 Machi 2018

Trump amfuta kazi Rex Tillerson na nafasi yake kumpa mkurugenzi wa CIA Mike Pompeo. Tillerson aliapishwa wadhifa huo Februari 2017. Aidha Trump amemteua Gina Haspel kama mwanamke wa kwanza kuwa mkurugenzi wa CIA.

https://p.dw.com/p/2uF4a
US-Außenminister Rex Tillerson
Picha: picture-alliance/dpa/J. Ernst

Rais wa Marekani Donald Trump Jumanne amesema amemfuta kazi Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson na nafasi yake inachukuliwa na mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA, Mike Pompeo. Aidha Trump amemteua Gina Haspel kuwa mkurugenzi wa CIA. Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

Ufutwaji huo wa kazi ni mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri la Trump tokea alipoingia madarakani na umekuwa ukitarajiwa  tokea Oktoba iliyopita baada kujitokeza ripoti zinazosema kuwa uhusiano umeharibika kati ya Trump na Tillerson, 65, ambaye aliacha kazi yake kama mtendaji mkuu wa kampuni ya simu ya Exxon ili kujiunga na utawala wa Trump.

"Mike Pompeo, Mkurugenzi wa CIA, atakuwa waziri mpya wa mambo ya nje. Atafanya kazi ya ajabu! Shukrani kwa Rex Tillerson kwa kazi yake! Gina Haspel atakuwa Mkurugenzi mpya wa CIA, na mwanamke wa kwanza kuwahi kuchaguliwa. Hongera kwa wote! " ameandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter.

Baadaye akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema Pompeo ni mtu anayemuamini na ambaye daima wamekuwa na mawazo yanayofanana.

Afisa mmoja wa ngazi za juu kwenye ikulu ya White House amesema Trump alikuwa amemuomba Tillerson mwenye ajiuzulu tangu Ijumaa, lakini hakutaka kutangaza wakati waziri huyo akiwa ziarani barani Afrika.

Tillerson hakuwahi kuiva chungu kimoja na Trump

Hata hivyo, taarifa nyengine zinasema kuwa Tillerson alikuwa hajui ikiwa angefutwa kazi wala sababu ya kuondolewa kwenye nafasi yake.

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo.
Waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. B. Ceneta

Kuondoka kwa Tillerson, mkuu wa zamani wa kampuni ya mafuta ya Exxon Mobil, kunatajwa kubashiri mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa baraza la mawaziri la Trump, na kilele cha mivutano kati ya wawili hao. 

Afisa huyo wa White House amesema Trump anaweza kufanya kazi vyema zaidi na Pompeo, mbunge wa zamani kutoka Kansas, ambaye anaonekana mtiifu kwake, na alimtaka awepo kabla ya mazungumzo yaliyopangwa kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, na majadiliano ya kibiashara.

Kwenye masuala kadhaa Tillerson, ambaye hakuwahi kushika nafasi yoyote ya kisiasa wala kidiplomasia kabla ya kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya kigeni, amekuwa na mawazo tafauti na bosi wake, yakiwemo masuala ya Korea Kaskazini na Urusi.

Hapo jana, Tillerson aliishutumu vikali Urusi kwa mashambulizi ya sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi na bintiye nchini Uingereza, ikiwa ni muda mchache baada ya msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders kukataa kuzungumzia hilo.

Hata hivyo, baadaye leo Trump naye alisema atazungumza na Waziri Mkuu wa Theresa May kuhusiana  na mashambulizi hayo, akikiri kuwa huenda Urusi ilihusika, ingawa hatoweza kutoa kauli rasmi hadi uchunguzi ufanyike.

Akizungumzia kufutwa kazi kwa Tillerson, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Michael Roth, amesema kuwa hatua hiyo haisaidii kurekebisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili. 

Mahusiano kati ya Marekani na washirika wake wengi wa Kimagharibi yamekuwa kwenye kipindi kigumu tangu kuingia madarakani kwa Trump mwaka jana.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman