1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aonesha matumaini baada ya UN kukutana na Jinping

Saumu Mwasimba
28 Machi 2018

Baada ya uongozi wa China na Korea Kaskazini kukutana,Trump aonekana kutiwa moyo na kuonesha kusubiri kwa hamu mkutano wake na Kim Jong UN wa korea Kaskazini

https://p.dw.com/p/2v9H2
Kim Jong Un in China
Picha: picture-alliance/XinHua/dpa/J. Peng

Baada ya Viongozi wakuu wa serikali wa China na Korea Kaskazini kukutana,rais wa Marekani DonaldTrump amesema kwamba mkutano wake na kiongozi wa jamhuri ya Korea Kaskazini Kim Jong Un utafanyika kama ulivyopangwa.Trump amesema kupitia  Twitta kwamba amepokea ujumbe jana usiku kutoka kwa mwenzake wa China Xi Jinping unaosema kwamba mkutano kati ya rais huyo wa China na Kim Jong Un ulikwenda vizuri na kwamba kiongozi huyo wa Korea Kaskazini anasubiri kwa hamu kukutana na Trump.

Baada ya siku mbili za kuendelea kwa eti eti kuhusu mkutano wa China na Korea Kaskazini ,hatimae China Jumatano ikatangaza kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliitembelea China na kukutana na mwenyeji wake Xi Jinping aliyekubaliana na Kim kwamba wataondowa silaha za Nuklea katika rasi ya Korea. Kutokana na taarifa hiyo rais wa Marekani Donald Trump ametangaza leo kupitia Twita kwamba amearifiwa juu ya ziara hiyo na kwamba yuko tayari kukutana na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kama anavyousubiri kwa hamu mkutano wake na Trump.

Donald Trump
Picha: Reuters/L. Millis

Pamoja na tamko hilo Trump ameongeza kusema kwamba kwa bahati mbaya kwa hivi sasa ni lazima vikwazo vikali na shinikizo viendelee kuwekwa kwa gharama zote dhidi ya nchi hiyo ya Korea Kaskazini. Ikulu ya Marekani jana ilisema kwamba China ilimpa maelezo Trump ya kilichoendelea katika mikutano ikiwemo ahadi ya kuondowa silaha za Nuklia ambayo imeonesha zaidi kwamba kampeini ya Marekani ya kuendelea kuishinikiza Korea Kaskazini inajenga mazingira mwafaka ya kuweza kufanyika mazungumzo na nchi hiyo.

Jumatano(28.03.2018) Trump ameandika kupitia Twita  kwamba kwa miaka kadhaa na kupitia serikali nyingi kila mmoja alikuwa akisema kwamba hakuna uwezekano wa kupatikana amani na kuondokana na silaha za Nuklia katika rasi ya Korea  lakini sasa kuna nafasi nzuri kwamba Kim Jong Un atafanya kile ambacho ni sahihi kwa ajili ya wananchi wake na kwa ajili ya ubinadamu.

Hata hivyo kuna viongozi wa nchi nyingine za ukanda huo wanaoiangalia hatua hii ya Kim Jong UN kwa tahadhari kubwa, kwa mfano waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe  ambaye amezungumza bungeni hii leo na kusema kwamba hakuna vikwazo vyovyote vya kibiashara dhidi ya Korea Kaskazini vitakavyoondolewa bila ya Pyongyang kuonesha hatua madhubuti:

''Serikali ya Japan inafuatilia hatua hii iliyopigwa kwa uangalifu mkubwa. na kwa hivi sasa tunakusanya taarifa pamoja na kuichambua hali ilivyo kwa sasa na tunatumai kupata ufafanuzi wa kueleweka kutoka upande wa China pia.''

Peking China Nordkorea Gespräche Xi Jinping Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/Xinhua/Y. Dawei

Ziara ya Kim China ni ya kwanza nje ya nchi yake kuwahi kujulikana tangu alipoingia madarakani 2011 na wadadisi wanaamini kwamba ni hatua inayolenga kuweka misingi ya maandalizi ya mikutano ya kilele inayokuja na Korea Kusini na Marekani.

Ikumbukwe kwamba mapema mwezi huu Trump aliushangaza ulimwengu kwa kukubali kukutana na Kim ingawa hadi sasa hijatajwa mkutano huo utafanyika lini na wapi. Mkuu wa usalama wa taifa wa Korea Kusini lakini amesema mkutano huo wa aina yake kati ya viongozi hao wawili huenda ukafanyika mwezi Mei japo maelezo kuhusu kinachoweza kujadiliwa hakijawekwa wazi na Ikulu ya White House imeshasema hicho kitafanyika ikiwa Korea Kaskazini itatizima ahadi ilizotowa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo