1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aonya uhamiaji haramu ni 'mzozo unaokuwa'

Grace Kabogo
9 Januari 2019

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema hali iliyopo katika mpaka wa Marekani na Mexico inazidi kuwa mbaya na imegeuka kuwa mzozo wa kibinaadamu.

https://p.dw.com/p/3BDvC
Präsident Trump spricht vom Oval Office aus die Nation zur Grenzsicherheit an
Picha: Getty Images/C. Barria-Pool

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema hali iliyopo katika mpaka wa Marekani na Mexico inazidi kuwa mbaya na imegeuka kuwa mzozo wa kibinaadamu.

 Akizungumza wakati akilihutubia taifa jana usiku katika Ikulu mjini Washington, amesisitiza kuwa hatua ya kushindwa kuwadhibiti wahamiaji haramu, inawaumiza mamilioni ya wananchi wa Marekani na kwamba mzozo wa kibinaadamu na kiusalama unaongezeka katika mpaka huo uliopo kusini mwa Marekani.

Amesema wahamiaji haramu ndiyo chanzo cha kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kinachoingizwa nchini humo pamoja na uhalifu, huku akiendelea kuitetea sera yake ya kuujenga ukuta kwenye mpaka huo.

Rais Trump ambaye ameitoa hotuba hiyo wakati ambapo bado kuna mkwamo wa shughuli katika baadhi ya idara za serikali ya Marekani, amesema kila siku maafisa wa forodha na walinzi wa mpakani wanakabiliana na maelfu ya wahamiaji haramu wanaojaribu kuingia nchini Marekani.

Washington  Chuck Schumer  Nancy Pelosi  PK nach Trump Treffen
Chuck Schumer na Nancy PelosiPicha: picture-alliance/CNP/M. H. Simon

''Kwa miaka mingi maelfu ya Wamarekani wameuawa kikatili na watu walioingia kinyume cha sheria nchini kwetu na maelfu ya maisha yatapotea tusipochukua hatua sasa. Huu ni mzozo wa kibinaadamu. Mwezi uliopita watoto wahamiaji 20,000 waliletwa kinyume cha sheria nchini Marekani, hilo ni ongezeko kubwa. Watoto hawa wanatumiwa na makundi katili ya uhalifu,'' alifafanua Trump.

Trump ambaye kesho anatarajiwa kuuzuru mpaka huo amewataka wabunge wa chama cha Democratic kuridhia kiasi cha Dola bilioni 5.7 za ujenzi wa ukuta katika mpaka huo. Amewaalika Wanachama wa chama hicho kurejea tena Ikulu ya White House hii leo kwa lengo la kukutana naye, akisema ni vibaya kwa wanasiasa kukaa kimya na kutochukua hatua yoyote. Trump amerudia wito wake wa kujengwa ukuta huo, akisema ni muhimu kwa ajili ya usalama.

Akimjibu Rais Trump, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi amemshutumu kiongozi huyo kwa kuishikilia serikali ya Marekani mateka na kuutengeneza mzozo kwenye mpaka huo. Pelosi ambaye aliongozana na Seneta Chuck Schumer katika kupeleka ujumbe wa wanasiasa wa Democratic, amemtaka Trump azifungue baadhi ya shughuli za serikali ambazo zimefungwa, akisema hatua hiyo haina maana yoyote na imesheheni taarifa zisizo sahihi kutoka kwa rais.

Mexiko Tijuana Migranten Träume & US-Pop Kultur
Muhamiaji akiwa kwenye mpaka kati ya Marekani na MexicoPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Schumer ambaye ni kiongozi wa Wademocrat walio wachache katika baraza la Seneti pamoja na Pelosi wamesisitiza kuwa wanaunga mkono usalama katika mpaka, lakini sio kwa kujenga ukuta utakaotumia gharama hizo kubwa na usio na manufaa.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kijasusi ya Baraza la Wawakilishi, Adam Schiff amesema katika historia ya Marekani, marais wameitumia Ikulu ya Marekani kuiunganisha nchi, lakini jana usiku Trump ameitumia ofisi hiyo kuchochea hofu na mgawanyiko.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DPA
Mhariri: Daniel Gakuba