1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump apindua wezani wa korti kuu ya Marekani

Oumilkheir Hamidou
1 Februari 2017

Donald Trump amemteuwa jaji Neil Gorsuch kuwa mjumbe wa korti kuu na kuwapa Republican fursa ya kuidhibiti taasisi hiyo muhimu . Maamuzi ya rais mpya wa Marekani yanaonyesha kuungwa mkono na wananchi wengi nchini humo.

https://p.dw.com/p/2WmDq
USA Trump Ernennung Neil Gorsuch
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Kaster

Katika taarifa yake kupitia televisheni jana usiku, rais Trump amewashituwa wamarekani kwa kumteuwa mwanasheria wa korti ya rufaa ya Denver, Colorado, mwenye umri wa miaka 49 kujaza pengo lililokuwepo katika korti kuu ya Marekani. Akiidhinishwa na baraza la Senet, Neil Gorsuch atajaza pengo lililoachwa kufuatia kifo cha Antonin Scalia takriban mwaka mmoja uliopita na kuupindua wezani kuwa wawakilishi watano wa Republican dhidi ya dhidi ya wanne, wa chama cha Democrats.

Kuteuliwa kwake kunaweza kushawishi maamuzi ya korti kuu ya Marekani katika kadhia kuanzia sheria za kibiashara, kupitia masuala ya jinsia hadi kufikia masuala ya haki ya kumiliki silaha.

Uteuzi wa Neil Gorsuch unazusha malalamiko miongoni mwa wamarekani. Kuna wanaodai amemteuwa kwasababu Neil Gorsuch ni miongoni mwa Wahafidhina waliobobea na waprotestanti waliomuunga mkono tangu dakika ya mwanzo alipoamua kugombea kiti cha rais.

Jaji mteule wea korti kuu ya Marekani
Jaji mteule wea korti kuu ya MarekaniPicha: Reuters/K. Lamarque

Neil Gorsuch ni mwanasheria mstahiki

Hata hivyo Melissa Hart, mhadhiri wa fani ya sheria katika chuo kikuu cha Colorado anahisi mwanasheria huyo anastahiki wadhifa huo: "Nnaamini ni mtu mwenye kufuata msimamo wake mwenyewe na mwelekeo wake wa kitaaluma kuhusu sheria. Hata kama sikubaliani nae kwa kila kitu lakini si mtu ambae yuko nje ya mkondo wa mambo, siamini, sawa na vile ambavyo siamini kama ni miongoni mwa wale wanaopitisha maamuzi bila ya kuzingatia misingi, bila ya kupima au kujali maisha ya watu. Nnaamini ni mtu ambae maamuzi yake ni yale ambayo tunayategemea kutoka kwa hakimu."

Wademocrats ambao ni wachache katika mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani Congress wanapinga kuteuliwa Gorsuch hasa baada ya wanachama wa Republican katika baraza la Senet kukataa kumidhinisha mteule wa Barack Obama Merrick Garland.

Wafuasi wa Donald Trump wadaai ukuta ujengwe
Wafuasi wa Donald Trump wadaai ukuta ujengwePicha: Getty Images/B. Mitchell

Idadi kubwa ya Republican wanauunga mkono maamuzi ya Donald Trump

Wakati huo huo uchunguzi wa maoni ya wananchi umebainisha laana za jumuia ya kimataifa,na maandamano , tahariri za magazeti na hotuba kali kali za wabunge dhidi ya maamuzi ya Donald Trump haziwashitui hata kidogo wafuasi wa Donald Trump. Uchunguzi huo umebainisha kwamba asili mia 80 ya Republicans waliunga mkono wiki iliyopita uamuzi wa rais mpya, ikiwa ni pamoja na kuzuwiliwa raia wa nchi sabaa za kiislam kuingia Marekani. Idadi sawa na hiyo wanaunga mkono pia ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga