1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema mtazamo wake kwa Syria umebadilika

Yusra Buwayhid
6 Aprili 2017

Urusi inakabiliana na ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa, kwa kuiunga mkono serikali ya Syria kufuatia shambulio la gesi ya sumu. Trump ametishia kuwa Marekani pekee inaweza kuishukulia hatua serikali ya Syria.

https://p.dw.com/p/2amKt
USA | Botschafterin der Vereinigten Staaten bei den Vereinten Nationen Nikki Haley mit Fotos syrischer Opfer
Picha: Reuters/S. Stapelton

Rais Trump alipoingia madarakani aliahidi kuimarisha ushirikiano na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Syria Bashar al-Assad. Trump alisema jitihada za Marekani nchini Syria zitalenga zaidi kupambana na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislam IS pekee.

Lakini baada ya kusambaa kwa vidio zinazoonesha watoto wa Syria wakitapatapa kama vile wamekwamwa koo, wakitokwa na mapovu ya mdomo na wakiwa katika maumivu makubwa sana... Trump alitangaza kuwa mtazamo wake juu ya mgogoro wa Syria umebadilika kutokana na shabulio hilo ambalo amelitaja kuwa halivumiliki na kwamba limevuka mipaka.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, ameonya kuwa Marekani inaweza kuchukua hatua peke yake.

"Umoja wa Mataifa unaposhindwa kutimiza jukumu lake la kuchukua hatua ya pamoja, kuna wakati tunahitajika kuchukua hatua wenyewe. Kwa maslahi ya waathirika, natumai baraza kwa ujumla lipo tayari kufanya hivyo. Dunia inahitaji kuona kwamba utumiaji wa silaha za kemikali haukubaliki," amesema Nikki Haley.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson imeisisitiza Urusi kufikiria tena ushirikiano wake na serikali ya Assad.

Syrien Idlib Giftgasangriff
Watoto wa Syria jimbo la IdlibPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/Syria Civil Defence

Onyo hilo la Marekani limekuja wakati wa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitishwa na Uingereza na Ufaransa, kufuatia shambulio hilo la Syria.

Serikali ya Syria hata hivyo imekana kuhusika na shambulio la gesi ya kemikali. Akiwa katika mkutano huo, Naibu Balozi wa Syria kwa Umoja wa Mataifa  Mounzer Mounzer amesema shutuma dhidi ya serikali ya Syria hazina msingi.

"Shutuma za kisiasa na zisizokuwa na msingi zimetolewa dhidi ya nchi yangu, Syria, na washirika wake katika vita vyetu dhidi ya ugaidi. Hivi ndivyo ilivyokuwa tangu siku ya kwanza, vyombo vya habari vinaripoti taarifa zilizotolewa na makundi ya kigaidi," Mounzer Mounzer.

Marekani, Ufaransa na Uingereza zimewasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kudai uchunguzi kamili kuhusu shambulio hilo linalotuhumiwa kuwa ni la silaha za sumu.

Wakishindwa kukubaliana juu ya rasimu hiyo, Urusi inaweza kutumia kura yake ya turufu kuizuia rasimu hiyo ya azimio. Urusi imeshawahi kutumia kura yake ya turufu mara saba kuilinda Syria dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa amesema rasimu ya azimio la nchi za Magharini imekosa umakini na haina ulazima, hata hivyo imekubali kufanyike uchunguzi.

Mandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape

Mhariri: Bruce Amani