1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asherehekea siku 100 madarakani

Sekione Kitojo
30 Aprili 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amesherehekea jana Jumamosi(29.04.2017), siku 100 akiwa madarakani katika Ikulu ya White House pamoja na kundi la watu wakimshangiria katika mkusanyiko unaofanana na mkutano wa kampeni.

https://p.dw.com/p/2c92Q
USA Harrisburg Trump Rede vor Anhängern
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP/C. Kaster

 akisifia  mafanikio yake  ya  mwanzo  na  kuwashambulia  wakosoaji  ambao  wametoa alama mbaya  kwa  utawaal  wake.

Trump  aliliambia  kundi  la  watu  waliokusanyika  kwamba  ndio  kwanza  anaanza  kutimiza ahadi  zake  za  wakati  wa  kampeni. Ameshambulia mara  kwa  mara  vyombo vya  habari alivyosema ,"havina uwezo, visivyokuwa  wa kweli" , akisema  havikuwa  vinasema  ukweli juu  ya  mafanikio  ya  utawala  wake.

"Utawala  wangu umekuwa  ukileta  mafanikio  kila  siku kwa  wananchi wa  nchi  hii," Trump alisema  mjini  Harrisburg, Pennsylvania. "Tunatimiza  ahadi  zetu  moja  baada  ya  nyingine, na  kwa  hakika  watu  wanafurahi  sana  juu  ya  hilo."

USA Neil Gorsuch
Jaji Neil Gorsuch wa mahakama kuu ya MarekaniPicha: Getty Images/D. Angerer

Mkutano  huo  ulifanyika  katika  siku  hiyo  hiyo  ambapo  maandamano  ya  mabadiliko  ya tabia  nchi  yalipofanyika  ambapo  maelfu  ya  waandamanaji  waliizunguka  Ikulu  ya  White House , na  pia  imeingiliana  na  hafla  ya  chakula  cha  usiku  kwa  ajili  ya  waandishi habari  kila  mwaka  maarufu  kama tai  nyeusi  katika Ikulu  ya  White  House  mjini Washington.

Trump  na  wafanyakazi  wake  waliamua  kutohudhuria  chakula  hicho  cha  usiku  na waandishi  habari kwasababu  ya  kile  alichosema  vyombo  vya  habari  kutomtendea   haki. Trump amesema  amejisikia  vizuri  kuwa  mbali  na  kile  alichokiita "kundi  la Washington", akiwa  na  maana  waandishi  habari.

Washington White House Correspondents' Association dinner Minhaj
Waandishi habari katika hafla ya chakula cha usiku mjini WashingtonPicha: Reuters/J. Ernst

"kundi  kubwa  la  wacheza  sinema  wa  Hollywood  pamoja  na  vyombo  vya  habari  mjini Washington wanajipongeza katika hafla  iliyotayarishwa  katika  hoteli  katika  mji  wetu  mkuu ," Trump  alisema  huku  kundi  hilo  la  watu  wakizomea. "Iwapo  kazi  ya  vyombo  vya habari ni  kuwa  waadilifu  na  kusema  ukweli, vyombo  vya  habari  vinastahili kipimo kikubwa  kabisa  cha  kushindwa.

Mafanikio ya  Trump

Trump aliorodhesha  kile  alichosema  ni  baadhi ya  mafanikio  yake  muhimu , ikiwa  ni pamoja  na  mafanikio  ya  kuthibitishwa kwa  jaji  wa  mahakama  kuu  Neil Gorsuch  na kusafisha  njia  kwa ajili  ya sheria  nyingine  nyingi  kuhusu mazingira  na  biashara.

Pia  ameorodhesha  idhinisho  lake  kwa  bomba  la  mafuta  la  Keystone XL  na  Dakota, akiuwa  makubaliano  ambayo  bado  hajaanza  ya  kibiashara  na  mataifa  ya  Asia, na kuimarisha  hatua  za  kiusalama  ambazo  zimesababisha  kupungua  kwa  kiasi  kikubwa kwa  watu   kuvuka  mipakani  kimagendo  katika  mpaka  wa  kusini.

Demonstrators gather for People's Climate March in Washington
Maandamano mjini Washington kupinga hatua anazochukua Trump kuhusu mazingiraPicha: Reuters/M. Theiler

"Dunia inapata ujumbe: Iwapo unajaribu  kuingia nchini  Marekani  kinyume  na  sheria , utakamatwa, kufungwa, kurejeshwa  nyumbani  kwenu  ama  kufungwa  gerezani," Trump alisema.

Amepuuzia  kushindwa  kwake  kupata  ushindi  muhimu  katika  ahadi  yake  ya  msingi wakati  wa  kampeni, kama  kuondoa  na  kuweka   mpango  mbadala  wa  sheria  ya matibabu  nafuu  pamoja  na  ujenzi  wa  ukuta  katika  mpaka  na  Mexico. Marufuku kwa wasafiri  wanaotembelea  nchini  Marekani  kutoka  mataifa  ya  Kiislamu  aliyojaribu  kuweka Trump , ilizuiwa  mahakamani.

Amewalaumu  Wademokrats kwa  kushindwa  sheria  hiyo  hadi  sasa  na  kusema  ahadi zake  zote  zitatimizwa  hatimaye.

"Tutajenga  ukuta jamani, wala  msiwe  na  wasi  wasi  juu  ya  hilo," amesema.

USA Harrisburg Trump Rede vor Anhängern
Rais Trump katika mkutano wake katika maonesho ya vifaa vya kilimo Pennsilvania MarekaniPicha: picture-alliance/AP/C. Kaster

Baadhi  ya  waungaji  wake  mkono  katika  kundi  hilo  la  watu  wamesema  wako  tayari kumpa  Trump  muda  zaidi.

"Nilimpigia  kura  na  nitampa  mwaka  mmoja. Inatosha  kuliweka  baraza  la  Congress katika  hali  bora  na  kuwezesha  baadhi  ya   mambo  kufanyika," amesema  Michael Casciaro , mwenye  umri  wa  miaka  54, mkandarasi  raia  katika  jeshi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri : Isaac Gamba