1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asifu uchumi wa Marekani Davos, akwepa tabianchi

Iddi Ssessanga
21 Januari 2020

Rais wa Marekani Donald Trump amejisifu kwa kuongoza mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini Marekani na kuutaka ulimwengu kuwekeza nchini humo. Alikuwa akuhutubia jukwaa la uchumi la dunia mjini Davos, Uswisi.

https://p.dw.com/p/3WaiJ
Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Picha: Reuters/J. Ernst

Trump ameuhutubia mkutano wa jukwaa la uchumi la dunia mjini Davos, saa chache kabla ya kuanza kesi ya kihistoria ya mashtaka dhidi yake katika baraza la seneti la bunge la Marekani mjini Washington.

Ziara hiyo ya siku mbili ya Trump itauweka katika majaribio uwezo wake wa kusawazisha hasira zake juu ya kushtakiwa na shauku ya kuonesha uongozi wake kwenye jukwaa la kimataifa.

Ameikumbusha hadhira kwamba alipozungumza kwenye jukwaa hilo miaka miwili iliyopita mwanzoni mwa kipindi chake cha urais, aliwaambia kuwa wamezindua mkakati kabambe wa kuirejesha Marekani kuwa taifa kubwa.

Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Rais Trump alipowasili Davos kwa ajili ya mkutano wa Jukwaa la kimataifa la uchumi, Januari 21,2020.Picha: Reuters/J. Ernst

"Ndoto ya Marekani imerudi ikiwa kubwa, bora na imara zaidi kuliko ilivyowahi kuwa. Hakuna anaenufaika kuliko Wamarekani wa tabaka la kati," alisema Trump.

Mchumi wa Kimarekani Kenneth Rogoff amesema baadhi lakini siyo madai yote ya Trump kuhusu nguvu ya uchumi wa Marekani ni sahihi. Lakini amebainisha kuwa uchumi haukuwa mbaya wakati alipoingia madarakani.

Akwepa kuzungumzia mabadiliko ya tabianchi

Rogoff amesema kuwa yumkini Trump amejihadhari kutoa matamshi kuhusu mabadiliko ya tabianchi kuepuka kuzomewa.

Mabadiliko ya Tabinachi ndiyo mada kuu ya mkutano wa mwaka huu na maneno ya "chukuwa hatua kuhusu tabianchi" yaliandikwa kwenye theluji katika eneo ambako helikopta ya Trump ilitua mjini Davos.

Hotuba ya Trump ilipokelewa kwa ukimya kutoka hadhira mbali ya ushangiliaji wa muda mfupi wakati Trump aliposema Marekani itajiunga na mkakati wa jukwaa la kiuchumi kupanda miti milioni moja kote duniani.

Kamishna Mkuu wa shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Filippo Grandi ameseka katika mkutano huo kwamba dunia inapaswa kujiandaa na uwezekano wa ongezeko la wakimbizi ambapo mamilioni ya watu watalaazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Mwanaharakati wa mazingira wa Sweden Greta Thunberg katika mojawapo ya vikao vya jukwaa la WEF, Januari 21, 2020.Picha: Reuters/D. Balibouse

Filippo amesema uamuzi wa Umoja wa Mataifa wiki hii unamaanisha wale wanaokimmbia kutokana na mabadiliko ya tabianchi wanapaswa kutendewa na nchi wenyeji kama wakimbizi, suala litakalokuwa na athari kubwa kwa serikali husika.

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa hukumu siku ya Jumatatu kuhusiana na loane Teitiota, kutoka taifa la pacifi la Kiribati, aliefungua kesi dhidi ya New Zealand baada ya mamlaka nchini humo kukataa madai yake ya ukimbizi.

Mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg amesema dunia bado haijapokea ujumbe kuhusu dharura ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kuwa kushindwa kwa viongozi wa dunia kuchukuwa hatua kunachochea moto kila saa inayopita.

Vyanzo: Mashirika