1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awasili Paris kufuatia mwaliko rasmi

John Juma
13 Julai 2017

Rais  wa  marekani Donald Trump  amewasili  mjini  Paris kwa  ziara  ya  siku  mbili  nchini  Ufaransa  ambapo  atakuwa  mgeni  rasmi katika  gwaride  la  kila  mwaka  la  siku  ya  Bastille.

https://p.dw.com/p/2gSRY
Frankreich Ankunft US-Präsident Donald Trump & Melania Trump
Picha: Reuters/K. Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump amewasili mjini Paris Ufaransa kwa ziara rasmi. Ziara hiyo inajiri siku ya sherehe ya kijeshi mjini Paris na Ikulu ya Marekani inatumai itampa Trump pumziko kidogo dhidi ya kashfa zinazomkabili nchini mwake.

Ndege iliyombeba rais Donald Trump Air Force One ilitua mjini Paris mapema leo, katika mwanzo wa ziara ya saa 24 ya Trump nchini Ufaransa kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron. Ziara hiyo inaenda sanjari na siku ya kitaifa ya Ufaransa hapo kesho ya kuadhimisha miaka 100 ya ushiriki wa Marekani katika vita vikuu vya kwanza vya dunia ambayo huwa na gwaride  la  kila  mwaka  la  siku  ya  Bastille.

Hii ikiwa mara ya kwanza kwa Trump kuzuru Ufaransa kama rais, inatarajiwa kuwa ziara hiyo itampa pumziko dhidi ya madai mazito yanayomzonga nchini mwake kuhusiana na tuhuma kuwa familia yake na wapambe wake walikuwa na mahusiano na Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Mswada wa kumuondoa Trump madarakani

Watalii karibu na mnara wa Eiffelturm mjini Paris
Watalii karibu na mnara wa Eiffelturm mjini ParisPicha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Kando na hayo ni kuwa hapo jana, mjumbe wa chama cha Democrat wa California Brad Sherman, alikuwa mbunge wa kwanza kuwasilisha rasmi mswada wa kutaka Trump aondolewe madarakani.

Sherman ametaja visa vya uhalifu mkubwa na mdogo mdogo kuwa sababu za kutaka Trump aondolewe madarakani, akisema juhudi za Trump kuzuwia uchunguzi juu ya uhusiano wa Urusi na iliyokuwa timu ya kampeni yake, pamoja na uchunguzi dhidi ya msaidizi wake mkuu, zinamaanisha alikusudia kuhujumu uchunguzi na haki.

Hata hivyo juhudi hizo huenda zikaambulia patupu kutokana na wabunge wa chama cha Republican kuwa wengi zaidi bungeni. Msemaji wa White House Sarah Huckabee alipoulizwa na mwanahabari kuhusu kauli yake kuhusiana na mswada huo aliipuuzilia mbali kuwa mchezo wa siasa. "Ninafikiri ni kichekesho sana na mchezo wa kisiasa unaochusha ahsanteni sana."

Katika ziara ya Ufaransa, mazungumzo kati ya Trump na Macron yanatarajiwa kulenga juhudi za pamoja za kulikabili kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria. Trump na Macron , wanataka  kuweka  kando tofauti zao  kuhusiana  na  biashara  na  mabadiliko  ya  tabia  nchi na  kupata  msimamo  wa  pamoja  watakapokutana  leo, kujaribu kupata suluhisho la  mzozo wa Syria pamoja  na  mikakati  mipana  zaidi katika  kupambana  na  ugaidi.

Rais Macron, Kansela Merkel na Rais Trump katika mkutano wa G20 Hamburg
Rais Macron, Kansela Merkel na Rais Trump katika mkutano wa G20 HamburgPicha: Reuters/J. Macdougall

Katika sherehe hizo muhimu za kuashiria wakati muhimu wa mageuzi ya Ufaransa, Trump atakuwa mgeni wa heshima, na pia atatembelea eneo alikozikwa aliyekuwa kiongozi wa kijeshi na kisiasa wa Ufaransa Napoleon. Trump  baadaye atalakiwa  kwa  heshima ya kijeshi katika Hoteli  des Invalides  mjini  Paris.

Wasiwasi wa viongozi dhidi ya Trump

Viongozi wa London, Berlin, Brussels, Paris na Ulaya wangali wanayo maswali kuhusu njia gani bora ya kushirikiana na Trump ambaye sera yake ya mfumo wa kuitenga Marekani imeathiri ushirikiano. Hata hivyo Macron anatumai kukuza uhusiano na Trump hali ambayo huenda ikamwezesha kushawishi sera za Marekani au kuepusha mikwaruzano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.

Ziara  ya  Trump  Paris,  ni  ya  pili  katika  bara  la  Ulaya  mwezi  huu  na  inakuja  huku  kukiwa  na  ufichuzi  mpya juu  ya  kampeni  yake ya kuwania urais. 

Wakati  huo  huo Kansela wa Ujerumani Angela  Merkel  na  rais wa  Ufaransa Emmanuel Macron  walifanya  mazungumzo pamoja  na  mawaziri  kutoka  nchi hizo mbili leo katika ikulu ya Ufaransa mjini Paris.
 

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE/

Mhariri: Iddi Ssessanga