1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ayataka mataifa ya Ulaya kuwapokea IS kutoka Syria

Sekione Kitojo
17 Februari 2019

Rais wa marekani Donald Trump jana Jumamosi alitaka mataifa ya Ulaya yawachukue mamia ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu  nchini Syria, akitishia kwamba Marekani bila hivyo italazimika kuwaachia huru.

https://p.dw.com/p/3DXBg
USA Rede Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

"Marekani  inazitaka  Uingereza, Ufaransa, Ujerumani  na  mataifa mengine   washirika  wa  Ulaya  kuwachukua  zaidi  ya  wapiganaji 800  ambao  wamekamatwa  nchini  Syria na  kuwafikisha mahakamani," rais  huyo  aliandoka  katika  mfululizo wa  maandishi yake  katika   ukurasa  wa  Twitter. "Eneo la  Ukhalifa linakaribia kuanguka. Mbadala  wake  sio  mzuri  kwa sababu  tutalazimika kuwaachia  huru.

Syrien YPG in Rakka
Wapiganaji wa kundi la Wakurdi la YPG nchini SyriaPicha: picture-alliance/dpa/S. Suna

"Marekani  haitaki  kuwa  walinzi  wa  wapiganaji  hawa  wa  ISIS kutoka  Ulaya, ambako  ndiko wanatarajiwa  kwenda.

"Tunafanya  mengi na tunatumia  fedha  nyingi, sasa  wakati  umefika kwa  wengine  kuchukua   jukumu  hilo na  kufanya  kazi  ambao wanaweza  sana  kuifanya. Tunaondoa  majeshi  yetu  baada  ya ushindi  wa  asilimia  100  dhidi  ya  sehemu  hiyo  ya  Ukhalifa!"

Maandishi  yake  katika  Twitter  yanakuja  baada  ya  makamu  wa rais Mike  Pence kutoa  wito  kwa  mataifa  mengine  kuchukua jukumu  nchini  Syria  wakati  vikosi vya  jeshi  la  Marekani vikiondolewa.

Pembezoni mwa  mkutano  wa  usalama  mjini  Munich, aliwaambia waandishi  habari kwamba  Marekani  inataka  mataifa  mengine kutoa vikosi vya  jeshi  na  mengine  vifaa  kusaidia  kuilinda  Syria.

Syrien Kämpfe gegen den IS
Wapiganaji wa Syria Democratic Forces wanaonekana wakiwa na mtu mmoja aliyejeruhiwa wakati wa mapambano na wanamgambo wa Dola la KiislamuPicha: Reuters/R. Said

Trump azusha wasi wasi

"Tunayaomba  mataifa  mengine  kujiunga nasi  na  kutupatia  vifaa na  msaada  na  vikosi vitakavyowezesha  kulinda  maeneo  na kuwazuwia  wapiganaji  wa  kundi  la  Dola  la  Kiislamu  ama  kundi lolote  la  itikadi  kali  kuweza  kuzuka  na  kuchukua  tena  maeneo yaliyokombolewa,"  amesema.

Trump  alisababisha  wasi  wasi  mkubwa  mwezi  Desemba  wakati ghalfa  alipotangaza  kwamba  Marekani  itaondoa  majeshi  yake kutoka  Syria  na  kwamba  kundi  linalojiita  Dola  la  Kiislamu  tayari limeshindwa.

Wakosoaji walionya  kwamba  kundi  hilo  la  kigaidi halijashindwa na  kumalizwa na  kwamba  kujiondoa  kwa  Marekani  kunaweza kusababisha  kufufuka  kwa  kundi  hilo, ambapo  washirika  wa Marekani  katika  eneo  hilo hawana  uwezo  wa  kupambana  na kitisho  hicho  peke  yao.

Majeshi  ya  kundi  la  Syrian Democratic Forces SDF , kundi  la wanamgambo   wanaoongozwa  na  Wakurdi  wakiungwa  mkono  na Marekani walianzisha  mashambulizi  wiki iliyopita  kuwaondoa wapiganaji  wa  kundi  la  Dola  la  Kiislamu  katika kijiji  cha  Baghuz, eneo  pekee lililoko  chini  ya  udhibiti wao, karibu  na  mpaka  na Iraq.

Syrien IS - Kampf um Baghus -  Zivilisten, die vor Kämpfen in der Nähe von Baghouz vor den Islamisten fliehen
Wanawake na watoto waliokimbia mapigano katika kijiji cha Bagouz, nchini SyriaPicha: Getty Images/C. McGrath

Pia  kuna  hofu kwamba  bila  ya  kuwapo  majeshi  ya  Marekani, Uturuki inaweza  kufanya  mashambulizi dhidi  ya  wanamgambo  wa SDF, ambao  wengi  wao  ni wapiganaji  wa  vikundi  vya  ulinzi  wa umma  vya  jamii  ya  Wakurdi  yaani  YPG.

Uturuki  inawaona  wapiganaji  hao  wa  YPG kuwa  ni  kundi linalotokana  na  kundi  linalotaka  kujitenga  nchini  Uturuki  la Workers' Party PKK, ambalo limepigana  vita  vya  miongo  kadhaa upande  wa  kusini  mwa  nchi  hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Zainab Aziz