1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuamua hatma ya wahamiaji watoto laki nane

Caro Robi
5 Septemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump atatangaza uamuzi wa iwapo atasitisha msamaha au la kwa maelfu ya watu walioingia Marekani kwa njia zisizo halali wakiwa watoto na ambao kwa kiasi kikubwa wametangamana vilivyo katika jamii

https://p.dw.com/p/2jMBM
USA Donald Trump unterzeichnet Dekret gegen Obamas Umweltspolitik
Picha: Reuters/C. Barria

Mtangulizi wa Trump, Barack Obama alitekeleza mpango wa kuahirisha hatua kuchukuliwa dhidi ya watoto wanaowasili Marakeni ujulikanao DACA miaka mitano iliyopita ili kuwasaidia wahamiaji hao ambao hawajafikisha umri wa utu uzima kuweza kuruhusiwa kusoma na kufanya kazi bila ya uoga.

Mjadala kuhusu mpango huo wa DACA umekuwa mkali kati ya pande zote mbili za kisiasa. Kwa siku kadhaa Ikulu ya Rais ya White House imesisitiza kuwa kuna njia nyingi ambazo zinazozingatiwa na kuonya dhidi ya kufanya mahitimisho ya kukurupuka kabla ya kutolewa tangazo rasmi.

USA Los Angeles - Demonstranten fordern den erhalt von DACA zum Schutz illegaler Immigranten
Waandamanaji wakiunga mkono mpango wa DACA nchini MarekaniPicha: Reuters/K. Grillot

Atatimiza ahadi au la?

Lakini ripoti zimekuwa zikiashiria kuwa Rais Trump ananuia kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeini kukomesha uhamiaji usio halali na kutia kikomo mpango huo wa DACA baada ya kuchelewa kwa miezi sita kutoa uamuzi ili kutoa fursa kwa bunge la marekani kupata suluhisho kuhusu hatma ya takriban wahamiaji 800,000 watoto ambao wengi wao ni kutoka nchi za Amerika Kusini.

Wabunge kadhaa wa Republican wameonya dhidi ya kuusitisha mpango huo maarufu moja kwa moja, uamuzi ambao huenda ukasabababisha kufurushwa kwa wengi wa watoto hao wajulikanao kwa jina maarufu 'Dreamers'.

Lakini uwezekano wa bunge ambalo limegawanyika vibaya kufikia muafaka kuhusu suala la uhamiaji ambalo limekosa muafaka kwa miaka kadhaa unaonekana kuwa finyu.

Licha ya matamshi makali wakati wa kampeni kuhusu uhamiaji, Trump amesema hadharani kuwa suala hilo linalowahusu wahamiaji waliongia Marekani wakiwa watoto kwa njia zisizo halali linamtia wasiwasi tangu alipoingia madarakani akiutaja uamuzi wake kuwa mmojawapo ya maamuzi magumu kumkabili na kuahidi ataushughulikia mpango wa DACA akiwa na kile alichokitaja kuwa moyo mkubwa.

Hatma ya watu laki nane mikononi mwa Trump

Akizungumza na wanahabari katika ofisi yake wiki iliyopita, alisema tunawapenda Dreamers akiongeza wanawapenda kila mtu. Washauri wa Trump wamedokeza kuwa maamuzi ya Rais yataongozwa na uzingativu wa kiuchumi.

USA Protest gegen Donald Trumps Einwanderungspolitik in New York
Wanaharakati waandamana kuwatetea wahamiajiPicha: picture-alliance/Zuma Press/Pacific Press/A. Lohr-Jones

Kellyanne Conway amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News kuwa Rais anataka kuwajali wafanyakazi Wamarekani, na kuzingatia maslahi ya watu wa Marekani wanaong'agania nafasi za ajira.

Kampuni nyingi za kibiashara hasa zile zilizoko katika sekta ya teknolojia zinapinga kufutiliwa mbali kwa mpango huo wa DACA ambao unawapa vibali vinavyoerefushwa kila baada ya miaka miwili wahamiaji ambao walikuwa chini ya umri wa miaka 16 walipowasili Marekani na ambao hawana rekodi ya kutenda uhalifu.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga