1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuelezea mafanikio yake kupitia hotuba kwa taifa

Sylvia Mwehozi
30 Januari 2018

Rais Donald Trump wa Marekani amesema hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa atakayoitoa usiku wa Jumanne,  itagusia mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha mwaka wake mmoja tangu aingie madarakani.

https://p.dw.com/p/2rmU3
USA Donald Trump erneuert Einreiseverbot
Picha: picture-alliance/dpa/NOTIMEX/Casa Blanca

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa, Trump amesema atazungumzia mada mbili  ikiwemo ukuaji wa uchumi na kupitishwa kwa maboresho ya sheria za kodi kwasababu ndio ajenda kuu pamoja na masuala ya uhamiaji na biashara.

"Tuna mengi ya kujadili na tutayajadili na natumaini kuwa mtafurahia", Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu baada ya hafla ya kuwaapisha wanachama wapya wa baraza lake la mawaziri.

Hotuba ya Trump ambayo inakuja baada ya hotuba yake ya kivitendo na yenye matumani katika kongamano la dunia la kiuchumi lililomalizika wiki iliyopita mjini Davos Uswisi, itaonyesha ukuaji wa uchumi wa Marekani na soko la hisa.

Aliwaeleza waliohudhuria Davos kwamba, mageuzi muhimu ya kupunguzwa kwa kodi yalikuwa ni historia kwa Marekani na akatoa wito wa kuondoa kanuni zisizohitajika, na kwamba wamevuka matarajio makubwa.

USA Präsident Trump und sein Sohn Donald Jr.
Mwaka mmoja uliopita Donald Trump alikula kiapoPicha: Reuters/C. Barria

Hotuba yake ya usiku wa Jumanne ina uwezekano wa kujumuisha sera ya uhamiaji kama ajenda kuu. Nchi hiyo imekuwa ikijadili suluhisho la uhamiaji haramu kwa miaka mingi bila ya mfanikio, alisema Trump na kuongeza kwamba anakusudia kufikia ufumbuzi unaounga mkono na vyama vyote vya siasa.

Trump amependekeza kuruhusu watu ambao waliletwa Marekani kinyume na sheria kama watoto kusalia nchini humo na kujipatia uraia kwa masharti ya kufadhili ujenzi wa ukuta katika mpaka wake na Mexico na makubaliano mengine.

"Bila shaka Wademocrats wataungana nasi ili tufanye jambo kubwa kwa ajili ya DACA, akimaanisha programu ya kushughulikia watoto wanaowasili na hoja ya kuhitajika kwa kura ya upinzani ili kupitisha sheria hiyo.

Trump alitangaza wiki iliyopita utayari wake wa kuongeza idadi ya watu watakaonufaika chini ya mpango huo anaopendekeza na kufikia milioni 2, lakini White House imesisitiza kuwa Trump badala yake anataka mabilioni ya dola katika ufadhili wa ujenzi wa ukuta.

Schweiz Weltwirtschaftsforum in Davos | US-Präsident Donald Trump
Trump akati wa kongamano la kiuchumi mjini Davos UswisiPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Trump pia anataka kusimamishwa kwa programu ya bahati nasibu ya visa ambayo bila mpangilio maalumu huwa inawapatia visa maelfu ya watu kila mwaka na kusimamishwa pia kwa "mnyororo wa wahamiaji" ambao unaruhusu mtu aliyepatiwa visa nafasi ya kuleta familia yake.

Anaweza kupongezwa pia kwa ongezeko la soko la hisa, ambalo Trump amesema ni jibu la moja kwa moja kwa sera yake rafiki ya biashara, hususan mswada wa kodi ambao alisaini kuwa sheria mwezi Desemba, na kuyaokoa makampuni ya Marekani katika kodi.

Pia atatoa msisitizo wa mikataba ya "biashara ya haki na ya usawa" na mafanikio katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu pamoja na kutoa wito wa haja ya matumizi makubwa katika miundombinu.

Kuelezea hayo, Trump amewaalika watu kadhaa kuhudhuria hotuba yake kama wageni wa heshima, amesema msemaji wa Ikulu Sarah Sanders . Miongoni mwao ni maveterani waliopoteza viungo wakati wakipigana nchini Iraq, watu waliosaidia katika athari za vimbunga na wazazi wa watoto waliouawa na genge la Ms-13.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman