1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuzungumza na Xi kuhusu vita vya kibiashara

Bruce Amani
29 Juni 2019

Vita vya kibiashara kati ya mataifa mawili makubwa kiuchumi vimefikia sehemu muhimu, wakati Rais Trump akikutana na mwenzake wa China Xi Jinping katika wakati ambapo pande zote zinaonyesha dhamira ya kuutuliza mzozo huo

https://p.dw.com/p/3LJPb
Japan Osaka | G20 Gipfel | Donald Trump und Xi Jinping
Picha: Reuters/K. Lamarque

Vita vya kibiashara kati ya mataifa mawili makubwa kiuchumi duniani vitafikia sehemu muhimu leo, wakati Rais Donald Trump atakutana na mwenzake wa China Xi Jinping katika wakati ambapo pande zote zinaonyesha dhamira ya kuutuliza mzozo huo uliodumu kwa mwaka mmoja, ijapokuwa hazionekana kutaka kufikia makubaliano.

Mkutano huo, ambao unafanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Kundi la G20 nchini Japan, ulikuwa ajenda muhimu ya siku nne za kidiplomasia kwa Trump. Akizungumza jana katika mkesha wa mkutano wao na Xi, Trump alisema kuwa anatumai mazungumzo yao yatatoa suluhisho la mzozo wa kibiashara.

Mkutano wake na Xi ni moja ya mitatu ambayo Trump anafanya leo na viongozi wa dunia wanaoonesha dalili za uongozi wa kimabavu. Atakutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salham na pia Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan

Trump amesema leo kuwa yuko tayari kukutana na Kim Jong Un katika eneo la mpakani lilisilokuwa na shughuli za kijeshi – DMZ kati ya Korea Kaskazini na Kusini. Trump alisema anaondoka leo kuelekea Korea Kusini kukutana na Rais wa nchi hiyo Moon Jae-in. Na kama Kim atakuwa na nia ya kukutana naye, basi yuko tayari kufanya hivyo