1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Kim kuanza mkutano wa pili wa kilele Vietnam

Bruce Amani
27 Februari 2019

Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jogn Un wanaanza mkutano wao wa pili wa kilele chini ya mwaka mmoja katika mji mkuu wa Vietnam Hanoi

https://p.dw.com/p/3E973
Vietnam Treffen Donald Trump und Kim Jong Un in Hanoi
Picha: Getty Images/AFP/M. Vatsyayana

Ikulu ya Marekani imesema Trump atakutana na Kim katika hoteli ya kihafari mjini Hanaoi ya Metropole iliyojengwa wakati wa enzi ya ukoloni wa Wafaransa na kufany mazungumzo ya ana kwa ana kwa dakik 20 kabla ya kushiriki hafla ya chakula cha jioni itakayodumu kwa saa moja na nusu.

Trump aliwasili jana mjini Hanoi kwenye ndege ya Air Force One. Na akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter. "Nimewasili Vietnam. Ahsanteni sana watu wote kwa makaribisho mjini Hanoi. Umati wa ajabu na upendo mkubwa”

Kim aliwasili kwa kutumia treni mapema jana, baada ya safari ya siku tatu ambayo ilikuwa ya umbali wa kilomita 3,000 kutoka mji mkuu wa Korea Kaskazini; Pyongyang, kupitia China. Alitumia sehemu ya mwisho ya safari yake kutoka mpaka wa Vietnam hadi Hanoi kwa kutumia gari.

Vietnam, Dong Dang: Staatsbesuch Kim Jong Un
Kim alisafiri kwa treni kutoka Pyongyang hadi VietnamPicha: Reuters/N. Sang

Viongozi hao wawili, ambao walionekana kuanzisha mahusiano mazuri na ya kushangaza katika mkutano wao wa kwanza wa kilele nchini Singapore Juni mwaka jana, wataandamana katika hafla ya chakula cha jioni na wasaidizi wawili na wakalimani, kabla ya kukutana tena kesho ALhamisi.

Mazungumzo yao yanakuja miezi minane baada ya mkutano wa kilele wa kihistoria nchini Singapore, ambao ulikuwa wa kwanza kati ya rais wa Marekani aliyeko madarakani na kiongozi wa Korea Kaskazini.

Wakati mkutano wa kwanza ulihusu kwa kiasi kikubwa kuanzisha mahusiano mazuri baada ya miongo mingi ya uhasama mkubwa kati ya nchi zao mbili, mara hii kutakuwa na shinikizo la kumtaka Kim kuenda mbali ya kutoa ahadi za maneno matupu na kuchukua hatua ya kuondoa kabisa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Wakosoaji wa Trump nyumbani wanamuonya dhidi ya kufikia mkataba ambao hautaweza kudhibiti mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini, na kumtaka ahakikishe kuwa nchi hiyo inatangaza hatua za kuaminika za kuwachana na silaha zake za nyuklia ambazo zinaitishia Marekani.

Singapur Gipfel Kim Jong Un Donald Trump
Kim na Trump walikutana Singapore mwaka janaPicha: Reuters/J. Ernst

Naye Kim atataraji kupata makubaliano muhimu na Marekani kama vile kuondolewa vikwazo vikali ilivyoekewa na tamko kuwa Vita vya Korea vya kati ya 1950 - 53 hatimaye vimemalizika rasmi. Kim aliandamana na dada yake, Kim Yo Jong, msaidizi wake muhimu.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani Mike Pompeo pia aliwasili jana na kukutana na mwenzake wa Vietnam Pham Binh Minh kwa mazungumzo.

Trump alisema kabla ya kuondoka Washington kuwa utakuwa mkutano mzuri sana wa kilele na akasisitiza kuhusu faida itakazopata Korea Kaskazini kama itawachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Wakati Marekani inaitaka Korea Kaskazini kuwachana kabisa na mipango yake ya nyuklia na makombora, Korea Kaskazini inataka kuona kuondolewa kwa mwamvuli wa nyuklia wa Marekani kwa Korea Kusini.

Safari ya Trump kutoka Washington inakuja wakati kukiwa na ongezeko la shinikizo nyumbani, na anataka kuonyesha mafanikio katika suala la sera ya kigeni ambayo iliwakabili watangulizi wake kadhaa.

Baadhi ya wachambuzi wanahofia kuwa hilo huenda likamfanya alegeze msimamo wake. Victor Cha, afisa wa zamani wa Ikulu ya White House aliyeshiriki mazungumzo ya Korea Kaskazini chini ya serikali zilizopita za Republican anasema wasiwasi mkubwa ni kama rais, akizungukwa na changamoto za nyumbani, atalegeza sana Kamba, na kupata mkataba mbaya ambao utaiacha Marekani na usalama mdogo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo