1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Moon kuijadili Korea Kaskazini

Amina Mjahid
22 Mei 2018

Rais wa Marekani Donald Trump atakutana kwa mazungumzo na rais wa Korea Kusini Moon Jae In katika ikulu ya white house, kujadili iwapo rais Trump atakutana na rais wa Korea Kaskazini katika mkutano wao mwezi ujao

https://p.dw.com/p/2y8Je
Südkorea Donald Trump und Moon Jae-in
Picha: Reuters/J. Ernst

Moon Jae In yupo ziarani nchini Marekani akiwa na lengo la kunusuru mkutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Korea Kaskazini uliyo mashakani muda mchache kabla ya kufanyika. Trump alikubali kukutana na Kim mjini Singapore tarehe 12 mwezi ujao, lakini mkutano huu wa kwanza kabisa kati ya marekani na korea kaskazini upo mashakani huku pande zote mbili zikionekana kutishia kutohudhuria mkutano huo unaolenga kuishawishi korea kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Tangu Marekani na Korea Kaskazini zilipokubali kukutana kumekuwepo na matukio ya kihistoria, kwanza ni ziara mbili za  Mike pompeo nchini humo kwanza kama mkurugenzi wa shirika la ujasusi CIA na pili kama waziri wa mambo ya nchi za nje  wa Marekani, pamoja na kuachiwa kwa raia watatu wa marekani waliyozuiwa korea kaskazini.

Korea-Gipfel 2018
Picha: Reuters

Lakini licha ya ushindi huo kwa serikali ya Trump, sasa hatua ya Korea Kaskazini ya kuachana na mpango wake wa nyuklia ipo mashakani.

Kwa sasa nchi hiyo iko katika hatua ya mwisho ya kuwa na teknolojia ya juu ya nyuklia na makombora itakayoiwezesha kuishambulia Marekani jambo ambalo Marekani inasema halitakubalika.

Marekani na Korea Kaskazini zatishia kutohudhuria mkutano wao wa kilele mwezi ujao

Mapema mwezi huu Korea Kaskazini  ilitupilia mbali moja ya masharti ya Marekani ya kutaka upande mmoja tu kuachana kabisa na mpango wa  nyuklia, na kufutilia mbali katika dakika za mwisho mkutano wake wa juu na Korea Kusini kufuatia zoezi la pamoja la kijeshi kati ya Korea Kaskazini na Marekani.

Baada ya tukio hilo Trump alijibu kwa kusema kuwa mkutano huo wa kilele kati yao huenda usifanyike. Hata hivyo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani mike pompeo akisema rais trump anaweza kujiondoa katika mazungumzo hayo huku akisema litakuwa kosa kubwa iwapo kim jong un atafikiriakuwa anaweza kumdhihaki rais Trump.

Wakati hayo yakijiri, afisa mkuu wa usalama wa Korea Kusini amesema hii leo kuwa ana matumaini ya asilimia 99.9 kwamba mkutano kati ya trumo na kim utafanyika. Chung Eui yong, ambaye ni mshauri mkuu kwa rais moon jae in licha ya kuwa na matumaini hayo amesema kwamba wanajiandaa kwa hali yoyote ile.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman