1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, Sanders washinda New Hampshire

10 Februari 2016

Donald Trump ameshinda uchaguzi wa kura ya maoni wa jimbo la New Hampshire kwa tiketi ya chama cha Republican huku Seneta Bernie Sanders akimpiga kumbo Hillary Clinton kwa upande wa chama cha Democratic.

https://p.dw.com/p/1HsUL
USA Bernie Sanders Donald Trump Kombo
Seneta Bernie Sanders (kushoto), mshindi wa Democratic na Donald Trump (kulia), alieshinda kwa upande wa Republican.Picha: Reuters/DW Montage

Wakionyesha kupoteza imani na mwelekeo wa uchumi na wanasiasa mjini Washington, wapigakura katika michuano miwili ya kwanza ya kura za mchujo kuelekea uchaguzi mkuu wa Marekani wamewaitikia kwa shauku kubwa wagombea wanaotazamwa kama wa nje ya mfumo.

Licha ya kuwa dhahiri, matokeo hayo hayakufanya vya kutosha kuondoa mchanganyiko kuhusu nani ataibuka kama mgombea mbadala kwa Donald Trump kwa upande wa chama cha Republican, huku kampeni ya mpinzani wa Sanders, waziri wa zamani wa mambo ya nje Hillary Clinton, wakipambana kujitetea kuhusu matarajio ya baadae.

Ushindi wa Trump unaimarisha hadhi yake ya mgombea wa usoni katika kinyanganyiro cha kumpata mgombea wa chama katika mbio za kumrithi rais Barack Obama katika Ikulu ya White House. Nyota huyo wa zamani wa vipindi vya uhalisia vya televisheni, ameshangiliwa na wafuasi wake kwa matamshi ambayo ambayo wengine wameyakosoa kuwa makosa kisiasa.

Wagombea wengine wa chama cha Republican, Ben Carson, Ted Cruz, Marco Rubio, Jeb Bush na John Kasich.
Wagombea wengine wa chama cha Republican (kutoka kushoto): Ben Carson, Ted Cruz, Marco Rubio, Jeb Bush na John Kasich.Picha: Imago

Kuendeleza mkakati wake wa ushari

Trump mwenye umri wa miaka 69 ameahidi kuwafukuza wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku kwa muda Waislamu kuingia nchini Marekani. Baada ya kushinda mbio hizo za New Hampshire, Trump aliwapongeza wagombea wengine lakini aliahidi kurudi kwenye makakati wake ushari baada ya ushindi huo.

"Laazima tuwashukuru wagombea kwa sababu wamepambana kweli na kupata ushindi dhidi ya baadhi yao, hata kama ni kwa wiki moja - lakini niaminini, itakuwa kwa wiki nyingi tu. Unajua mara zote ni ngumu lakini baada ya hapo, kesho itakuwa boom boom. Lakini hivyo ndivyo ilivyo, na kiukweli tuna vipaji ndani ya chama cha Republican," alisema Trump.

Trump alikuwa wa kwanza kwa kupata asilimia 34 ya kura, akifuatiwa na gavana wa jimbo la Ohio John Kasich aliepata asilimia 16. Gavana wa zamani w ajimbo la Florida Jebb Bush alikuwa akichuana katika nafasi ya tatu na seneta wa Florida Marco Rubio pamoja na Ted Cruz, alisehinda kura ya wiki iliyopita jimboni Iowa.

Sanders vigelegele, Clinton ajitetea

Kwa upande wa chama cha Democrats, Bernie Sanders alipata asilimia 60 dhidi ya 38 za Clinton, ambaye kwa miezi kadhaa alikuwa akiongoza katika uchunguzi wa maoni kitaifa. Sanders ambaye amejitaja kuwa msoshalisti asietaka ufadhili wowote kutoka kwa makundi ya kibiashara, ameahidi kujenga uchumi unaowanufasiha Wamarekani wote na siyo asilimia moja tu ya matajiri.

Sanders na Hillary Clinton wakiteta jambo baada ya mmoja ya midahalo yao ya Televisheni hivi karibuni.
Sanders na Hillary Clinton wakiteta jambo baada ya mmoja ya midahalo yao ya Televisheni hivi karibuni.Picha: picture-alliance/dpa/M. Nelson

"Leo tumetuma ujumbe utakaosikika kuanzia Wall Street hadi Washington, kuanzia Maine hadi California, na ujumbe huo ni kwamba serikali ya taifa letu kubwa ni ya watu wote na siyo ya matajiri wachache tu wanaochangia kampeni na kamati za ushawishi," alisema Sanders huku akipigiwa vifijo na vigelegele.

Clinton mwenye umri wa miaka 68, alimpongeza Sanders mwenye umri wa miaka 74 katika hotuba kwa wafuasi wake, na kutetea misimamo yake yenye kuendelea na kuapa kuwa mgombea anaetatua matatizo na siyo kuyataja tu.

Aliwatolea mwito wapigakura wenye asili ya Afrika pamoja na Walatino na kukiri kuwa alikuwa na kazi kubwa ya kufanya kuwashamishi wapigakura vijana.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Grace Kabogo