1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi apinga mageuzi ya mahakama Congo

Saleh Mwanamilongo
30 Juni 2020

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi amesema hawezi kukubali mabadaliko yoyote yatakayodhoofisha uhuru wa mhimili wa kisheria nchini mwake, baada ya muungano wa FCC kupendekeza mabadiliko ya sheria.

https://p.dw.com/p/3eZ5c
Demokratische Republik Kongo Kinshasa | Präsidenten | Fotomontage
Picha: G. Kusema

   Kwenye hotuba yake rais Tshisekedi anasema kwamba hakuna chama cha kisiasa au kundi la watu ambalo lina mamlaka dhidi ya misingi ya kikatiba.

''Siwezi kukubali kwa sababu zozote zile mageuzi kwenye sekta hiyo ambayo kwa aina moja au nyingine yanaweza kuhujumu misingi ya uhuru wa kisheria kama ilivyo hivi sasa ndani ya katiba yetu,'' alifafanua Rais Tshisekedi.

Matamshi yake yametolewa baada ya siku kadhaa ya mvutano mkali wa kisiasa na maandamano mjini Kinshasa wa kupinga mageuzi ya kisheria yaliyopendekezwa na wabunge kutoka vuguvugu la kisiasa la FCC, la rais wa zamani Joseph Kabila.

Tshisekedi anasema miaka 60 baada ya uhuru, Congo haijapiga hatua nzuri ya maendeleo, huku akiwanyooshea kidole cha lawama wanasiasa ambao toka uhuru waliyapa kipaumbele maslahi yao binafsi na kusahau yale ya wananchi.

DR Kongo Kinshasa | Protest & Demonstration
Wandamanaji wengi wao wakiwa waendesha pikipiki wakiwa wamebeba bango la kupinga kuingiliwa idara ya mahakama mjini Kinshasa.Picha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Rais akosolewa kwa kuchukuwa upande

Hata hivyo, hotuba hiyo ya Rais Tshisekedi imekosolewa na baadhi ya wananchi ambao wanahisi kwamba amejiingiza katika mzozo wa kisaiasa baina ya chama chake na kile cha mtangulizi wake.

Dieudonne Mushagalusa, mratibu wa asasi za kiraia nchini Congo, anahisi kwamba Rais Tshisekedi alitakiwa kutoegemea upande wowote.

''Rais anatakiwa kutoegemea upande wowote na ikiwa kuna tofauti baina ya bunge na vyombo vya kisheria ni rais anmabae anatakiwa kuingilia kati ilikuhakikisha uhuru wa kila taasisi''.

 Aidha, Rais Tshisekedi alisisitiza nia yake ya kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na vuguvugu la FCC, na amewataka wanasiasa wote kuwa na mshikamano wa kitaifa mnamo kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.

Rais Tshisekedi ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, aliingia katika maelewano na chama cha FCC cha rais wa zamani wa Congom,Joseph Kabila, kushirikiana naye katika serikali yake, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.

Belgien König Philippe Flagge
Mfalme Philippe wa Ubegiji amemuandikia barua rais Felix Tshisekedi kuomba radhi kwa madhila waliopitia raia wa Jamhuri ya sasa Kidemokrasi ya Congo wakati wa utawala wa kikoloni wa Ubelgiji.Picha: picture-alliance/dpa/P. van Katwijk

Mfalme Ubelgiji ajutia mateso wakati wa ukoloni

Kwa upande mwingine Mfalme Phillipe wa Ubelgiji ameelezea majuto yake kwa madhara yaliyosababishwa na ukoloni wa nchi yake nchini Kongo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa utawala wa Ubelgiji kutamka kauli kama hiyo.

Katika barua yake aliyompelekea Rais Felix Tshisekedi hivi leo katika siku ambayo Kongo inaadhimisha miaka 60 ya kumalizika kwa ukoloni wa Ubelgiji, Mfalme Phillipe amesema anajutia majeraha ya kale ambayo maumivu yake yapo hadi leo kutokana na ubaguzi unaoendelea kwenye jamii.

Wanahistoria wanasema mamilioni ya Wakongo waliuawa, kukatwa viungo vyao ama kufa kwa maradhi wakati wakifanyishwa kazi kwenye mashamba ya mpira yaliyokuwa yakimilikiwa na Mfalme Leopold II wa Ubelgiji.

Bila ya kumtaja babu yake huyo mkuu kwa jina, Mfalme Phillipe ameandika kwenye barua hiyo kwamba matendo ya ukatili na unyama yaliyofanywa wakati huo ni sehemu kubwa ya kumbukumbu za pamoja kati ya Kongo na Ubelgiji.

Masanamu kadhaa ya Leopold, aliyetawala baina ya mwaka 1865 na 1909, yamechafuliwa kwa rangi au kuvunjwa na waandamanaji nchini Ubelgiji katika siku za hivi karibuni, katika wimbi la hasira lililochochewa na mauaji ya Mmarekani Mweusi George Floyd mwezi uliopita akiwa mikononi mwa polisi wa Minneapolis, Marekani.

Chanzo: Mashirika