1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Abbottabad yafichua maisha ya Bin Laden

Josephat Nyiro Charo9 Julai 2013

Osama bin Laden aliishi kama mtu wa kawaida bila wasiwasi wowote kwa karibu miaka 10 na aliwahi hata kusimamishwa na polisi katika eneo la Swat huko Pakistan kwa kupeleka gari kwa kasi mno, lakini hakukamatwa.

https://p.dw.com/p/194Ew
FILE - This April 1998 file photo shows exiled al Qaida leader Osama bin Laden in Afghanistan. Al-Qaida's image was a top concern on Osama bin Laden's mind in the last months of his life. In letters captured in the U.S. raid that killed him, the terror leader complains that al-Qaida branches kill too many Muslim civilians, turning the public against them. He was angered the would-be Times Square bomber broke his U.S. citizenship oath not to harm the United States. "We do not want the mujahedeen to be accused of breaking an oath," bin Laden wrote. (AP Photo, File)
Osama bin LadenPicha: AP

Ripoti hiyo iliyofichuliwa kwa televisheni ya al Jazeera na kuonyeshwa Jumatatu jioni (08.07.2013), inaonyesha kinaganaga maelezo ya kusisimua kuhusu maisha ya Osama bin Laden, mtu hatari aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, na aliyekuwa akivaa kofia la mchunga ng'ombe katika tambarare za Marekani, kuepuka kugunduliwa kutoka angani.

Ripoti hiyo ya kurasa 336, iliandikwa na tume ya Abbottabad inayoongozwa na jaji na iliyoundwa na serikali ya Pakistan muda mfupi baada ya vikosi maalumu vya Marekani kumuua bin Laden Mei 2 mwaka 2011. Misingi ya ripoti hiyo ni mahojiano yaliyofanywa na vyanzo 201, wakiwemo jamaa wa familia yake na maafisa mbalimbali.

Matokeo ya uchunguzi huo ambayo hayajachapishwa rasmi, yanajumuisha ushahidi wa uzembe mkubwa katika karibu kila ngazi ya vyombo vya usalama vya Pakistan. Ripoti inakosoa vikali namna Marekani ilivyofanya uvamizi katika makazi ya bin Laden huko Abbottabad, ikisema ilichukua hatua kama jambazi mhalifu. Inauweka katika kiti moto utawala wa Pakistan kwa kushindwa kugundua shughuli za shirika la ujasusi la Marekani, CIA, katika ardhi yake, na hautupilii mbali uwezekano wa kuhusika maafisa walaghai katika idara ya ujasusi ya Pakistan, suala tete kuligusia katika uchunguzi wa hali ya juu namna hiyo.

Osama aliingia Pakistan akitokea Afghanistan

Ripoti inatoa maelezo kuhusu usiku wa kifo cha bin Laden na kutoa taswira ya mtu aliyekuwa akibabakia na kama mwenda wazimu ambaye kila mara alikuwa mbioni kukwepa kutiwa mbaroni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Bin Laden aliwasili nchini Pakistan msimu wa machipuko mnamo mwaka 2002, na wakati mmoja aliishi Haripur kwa miaka miwili kabla kuhamia katika makazi yake ya mjini Abbottabad na familia yake kubwa mnamo mwezi Agosti mwaka 2005. Ripoti inasema maeneo yote alikoishi hayajulikani kikamilifu, lakini miongoni mwao ni FATA yani Waziristan kusini na Bajaur, Peshwar, Swat na Haripur.

Pilzförmige Rauchwolken steigen am 13.12.2001 nach massivem US-Bombardement auf die Tora-Bora-Region im Osten Afghanistans auf. Afghanische Stammeskämpfer haben nach eigenen Angaben die Terrororganisation El Kaida aus den ostafghanischen Bergen von Tora Bora vertrieben.
Eneo la Tora Bora, AfghanistanPicha: dpa

Ripoti imegundua bin Laden aliingia Pakistan akitoa eneo la Tora Bora nchini Afghanistan, ambako majeshi ya Marekani yalikuwa yakimsaka mwaka 2002. Familia yake ilihamia Karachi, Pakistan kutoka Kandahar, muda mfupi baada ya mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani dhidi ya jengo la shirika la biashara la kimataifa, WTO mjini New York, makao makuu ya wizara ya ulinzi, Pentagon nje ya mji wa Washington, na uwanja mmoja huko Pennsylvania.

Osama hakupenda mali

Katika ushuhuda wao wake wa bin Laden walisema hakupenda sana mali zake binafasi na alikuwa na nguo chache sana. Ripoti hiyo imesema kabla kwenda Abbottabad bin Laden alikuwa na mavazi matatu ya kitamaduni yajulikanayo kama shalwar kameez aliyoyavaa wakati wa msimu wa kiangazi na mengine matatu kwa ajili ya msimu wa baridi. Wakati alipojihisi anaugua, Osama bin Laden alijitibu mwenyewe kutumia dawa za kienyeji za kiarabu. Kwa mujibu wa ripoti zisizo rasmi za Marekani, bin Laden alikuwa akiugua ugonjwa wa Addison, upungufu wa adrenalini mwilini, na kila mara alipojihisi mvivu angekula tufaha na chokoleti.

Maafisa wa serikali na usalama nchini Pakistan hawakuweza kupatikana ili kutoa kauli kuhusu ripoti hiyo. Baadhi ya maafisa wa Marekani wameelezea wasiwasi wao wakiyashuku mashirika ya ujasusi ya Pakistan kwa kumlinda bin Laden, lakini Pakistan imelipuuzilia mbali wazo hilo.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman