1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Ivory Coast yachagizwa kutangaza matokeo

2 Desemba 2010

Siku ya mwisho iliyotolewa ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Ivory coast imepita pasi matokeo hayo kutangazwa na tume huru ya uchaguzi nchini humo.

https://p.dw.com/p/QNnR
Wananchi wakisubiri kupiga kura kwenye uchaguzi wa Jumapili iliyopita nchini Ivory CoastPicha: AP

Na sasa hali ya wasiwasi inazidi katika nchi hiyo ambapo zaidi ya watu 10 wamefariki katika vurugu zinazosemekana kuzuka kufuatia awamu hiyo ya pili ya uchaguzi.

Tume huru ya uchaguzi nchini Ivory Coast,CEI, ilitakikana kuanza kutoa matokeo ya uchaguzi huo lakini muda wa mwisho uliotolewa, ulipita pasi matokeo hayo kutangazwa.

Chama tawala kinasemekana kulalamikia matokeo katika maeneo manne Kaskazini.

Präsidentschaftswahlen Elfenbeinküste Laurent Gbagbo
Rais Laurent GbagboPicha: picture alliance/PANAPRESS/MAXPPP

Rais Laurent Gbagbo amekilaumu kikosi cha waliokuwa waasi kutoka kaskazini,wanaomuunga mkono Alassane Outtara kwa kuwanyanyasa wafuasi wake na ametaka tume hiyo ya uchaguzi kufutilia mbali matokeo ambayo hayajawasilishwa mpaka sasa.

Wakati huo huo mkuu wa kampeni za Outtara, ametoa malalamiko kama hayo ya kunyanyaswa kwa wafuasi wa Outtara katika maeneo yalio na wafuasi wengi wa Gbagbo.

Kwa mujibu wa kituo kimoja cha redio ya kimataifa, Msemaji wa tume hiyo huru ya uchaguzi, Bamba Yacouba, anasemekana alikuwa akijitayarisha kutangaza matokeo ya maeneo matatu kati ya 18, wakati wafuasi wawili wa rais Laurent Gbagbo walimpokonya na kuziraruwa karatasi za matokeo hayo wakidai kwamba sio ya kweli.

Rais Gbagbo na Outtara ambaye alikuwa waziri mkuu na afisa mkuu katika shirika la kimataifa la fedha IMF, walishindana katika uchaguzi ambao unanuiwa kusitisha vita vya kiraia vya mwaka 2002, vilivyoigawanya nchi hiyo pande mbili, kaskazini uliyo na idadi kubwa ya waislamu, na kusini uliyo na wakristo wengi.

Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ametoa wito wa tume hiyo huru kupewa muda na nafasi muafaka kuyashughulikia matokeo hayo ya uchaguzi.

Katika taarifa yake, katibu huyo mkuu amewaomba washika dau wote nchini humo na taasisi mbali mbali, kuwajibika na kujizuia kufanya vurugu hadi matokeo yatakapo tangazwa .

Kuchelewa kutolewa kwa matokeo hayo na hali ya kutokuwa na imani nayo kunazusha wasiwasi katika taifa hilo lililopo Magharibi mwa Afrika.

Mkuu wa shirika la kuetetea haki za binaadamu la Umoja wa mataifa, Navi Pillay amewaonya viongozi hao wakuu wa Ivory Coast, kwamba watalaumiwa kwa vurugu zozote wafuasi wao watakazozusha.

Ufaransa na Marekani zimewaomba Gbagbo na Outtara kukubali matokeo yatakayotolewa ya uchaguzi huo, ambapo mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini humo, Choi Young-jin, ameutaja kuwa uchaguzi wa kiwango kikubwa cha demokrasia.

´´Kila kitu kilifanyika sawa na utaratibu ulikuwa mzuri.Tumefanya kila kitu kwa mujibu wa inavyotakiwa´´

Rais Gbagbo alishinda asilimia 38 ya kura huku Outtara akishinda asilimia 32 katika awamu ya kwanza ya kura hizo mnamo tarehe 31 mwezi Oktoba.

Uchaguzi huo wa rais umeahirishwa mara sita tangu mwaka 2005.

Mwandishi Maryam Abdalla/DPAE

Mhariri:Aboubakary Liongo