1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunaishi katika dunia ya utawala wa ubaguzi wa kiuchumi.

Mohamed Dahman13 Mei 2007

Zimebakia pungufu ya wiki mbili kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Baraza la Saba Duniani la CIVICUS Muungano wa Dunia wa Ushiriki wa Raia.Chombo hicho chenye makao yake makuu mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini hujumuisha pamoja mashirika yasio ya kiserikali kutoka duniani kote kuimarisha mashirika ya kijamii hususan pale harakati zao zinapotishiwa.

https://p.dw.com/p/CHky

Mkutano huo wa tarehe 23 hadi 27 mwezi wa Mei utafanyika mjini Glasgow Scotland.Mji huo ulifanyika mkutano wa baraza hilo mwaka jana na pia utakuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka 2008.Mikutano ya baraza hilo ya mwaka 2006,2007 na 2008 pia mada yake ni moja : Kuchukuwa hatua ya pamoja kwa ajili ya kuwa na dunia yenye haki.

Katibu Mkuu wa CIVICUS Muungano wa Dunia wa Ushiriki wa Raia Kumi Naidoo alizungumza na shirikia la habari la IPS kuhusu harakati za muungano wao ambapo alielezea pamoja na mambo mengine juu ya uamuzi wao wa kuendelea kushikilia mada hiyo hiyo katika mkutano wao.

Naidoo amesema dunia imekuwa ikisambaratika baada ya kuungana ambapo kwa hivi sasa kunajitokeza mapungufu chungu nzima ikiwa ni pamoja na kuzidi kugawika kwa nchi za Kusini na Kaskazini yaani zile za kimaskini na kitajiri,utengano katika kanda nao pia umekuwa ukizidi kuimarika halikadhalika kuongezeka kwa mizozo ya ndani ya nchi jambo ambalo limefanya mada hiyo ya kuchukuwa hatua kwa pamoja kwa ajili ya kuwa na dunia yenye haki kuwa ni muhimu na isiopitwa na wakati.

Asilimia hamsini ya mashirika yasio ya kiserikali yanatazamiwa kuwakilishwa tena katika mkutano huo wa Glasgow juu ya kwamba matumaini ya Muungano wa Dunia kwa Ushirika wa Raia ni kuwa na washiriki tafauti yaani sura mpya ili kwamba waweze kujenga uhusiano wao kwa mapana zaidi.

Kuhusiana na idadi inategemewa itakuwa kama ilivyokuwa mwaka ajana wakati takriban watu 600 kutoka nchi 110 duniani walihudhuria.

Ujumbe unaotarajiwa kutolewa na muungano huo kwa mkutano wa viongozi wa Kundi la Mataifa Manane lenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani nchini Ujerumani hapo mwezi wa Juni utakita katika masuala ya kufuta madeni, kuboresha kiwango cha misaada na kuongeza misaada yenyewe,haki katika biashara, usawa wa kijinsia,rushwa na utawala bora.

Ni miaka miwili tu iliopita huko huko Scotland katika mji wa Gleangles viongozi wa Kundi la Mataifa Manane walitowa hadi nzuri kem kem.Katika suala la kufuta madeni walifuta madeni ya nchi 14 za Kiafrika na nchi nne za Amerika ya Kusini.Muungano wa Dunia kwa Ushiriki wa Raia CIVICUS ulikuwa unataka nchi 46 zifaidike na makubaliano ya viongozi wa Kundi la Mataifa Manane.

CIVICUS inaona kwamba Kundi la Mataifa Manane limekuwa likiburuza miguu katika mazungumzo ya biashara na kuzingatia zaidi maslahi ya kichoyo ya nchi zao.Mfano ni kwa wafugaji wa Ulaya kupeleka biashara ya nyama ya kuu kwa bei ya kutupwa nchini Ghana kiasi cha kuwafanya wafugaji wa Ghana kuvurugikiwa katika soko lao wenyewe la taifa.

Kwa maoni ya Katibu Mkuu wa CIVICUS Kumi Naidoo wanaishi katika dunia ya utawala wa ubaguzi wa kiuchumi na huo ndio aina ya ujumbe watakouwasilisha kwa Kundi la Mataifa Manane.

Na kama ilivyokuwa kwa mwaka jana mkutano wao pia utalenga wanaharakati wa mashirika ya kijamii ambao wako gerezani kwa kutaja mifano ya watu 20 kutoka sehemu mbali ili kuonyesha kwamba jambo hilo linatendeka duniani kote.

Halikadhalika jinsi vita vya ugaidi vilivyokuwa na taathira mbaya kabisa kwa demokrasia kwa jumla na hususan katika nafasi ya mashirika ya kijamii.