1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia maandamano yaendelea

Sekione Kitojo23 Januari 2011

Polisi wameshiriki katika maandamano nchini Tunisia, wakisema kuwa wanawajibika kwa wananchi.

https://p.dw.com/p/10185
Waandamanaji wakiimba kauli mbiu za kumtaka waziri mkuu Ghannouchi kujiuzulu mjini Tunis.Picha: dapd

Waandamanaji nchini Tunisia wamedai kuondoka madarakani kwa waziri mkuu jana na mchunguzi mmoja ameahidi kufichua jukumu la wizara ya mambo ya ndani katika kushambuliwa kwa risasi kwa watu kadha waliokuwa wakiandamana. Wakitiwa nguvu na kuondoka madarakani kwa rais wa nchi hiyo wiki moja iliyopita, katika mapinduzi ya Jasmini, waandamanaji waliingia mitaani kujaribu kulazimisha kuondolewa kwa wafuasi wake serikalini.

Wakiwa hawaridhishwi na ahadi yake ya kuondoka madarakani mara uchaguzi huru utakapofanyika, mamia ya waandamanaji walipita kwa nguvu katika uzio uliowekwa na polisi katika ofisi ya waziri mkuu Mohamed Ghannouchi. Siku ya Ijumaa, Ghannouchi aliyebaki kuiongoza serikali ya mpito , baada ya rais Zine al-Abidine Ben Ali kukimbia hapo Januari 14, ametoa wito wa uvumilivu.

Lakini wakati akikutana na baraza jipya la mawaziri jana Jumamosi , maelfu ya watu waliandamana ikiwa ni pamoja na polisi wa nchi hiyo.