1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tusk achaguliwa tena urais wa EU

Mohammed Khelef
10 Machi 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemchaguwa tena Donald Tusk kuwa rais wao, licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa nchi yake mwenyewe, Poland, inayoonya dhidi ya tabia ya ubabe Ujerumani kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2YwZt
Polen Donald Tusk
Picha: picture alliance/dpa/A. Vitvitsky/Sputnik

Viongozi hao walipiga kura 27 dhidi ya moja tu kwenye mkutano wa kilele mjini Brussels hapo jana, uchaguzi unaomfanya waziri mkuu huyo wa zamani wa Poland kupata nafasi ya kuhudumu tena kwa mwaka miwili na nusu kwenye wadhifa huo wa rais wa Umoja wa Ulaya. 

Kura pekee ya kumpinga Tusk ilipigwa na Waziri Mkuu wa Poland, Beata Szyldo, ambaye chama chake cha siasa kali za mrengo wa kulia, Law and Justice, kimekuwa na mzozo wa muda mrefu na Tusk, anayefuata siasa za wastani.

Haraka baada ya kura hiyo, Szyldo alisema hakubaliani nayo na kwamba atayapigia kura ya turufu, akihoji uhalali wa kumchaguwa mtu ambaye haungwi mkono na nchi yake mwenyewe.

"Kwanza Tusk hahakikishi kwamba haegemi upande wowote, rais wa Baraza la Ulaya hatakiwi kushiriki siasa na hawezi kuwa upande mmoja wa kisiasa, kwenye mgogoro wa ndani. Hawezi kushirikiana na upinzani na kupambana na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia", alisema waziri mkuu huyo.

Brüssel - EU -Gipfel - Beata Szydlo
Waziri Mkuu wa Poland, Beata Szyldo, anaamini Donald Tusk hafai kuuongoza Umoja wa Ulaya kwa kuwa anajihusisha na siasa za ndani za Poland, alikowahi kuwa waziri mkuu.Picha: picture alliance/dpa/Belga/T. Roge

Waziri wake wa mambo ya nje, Witold Waszczykowski, alisema baada ya uchaguzi wa Tusk kwamba Poland inatambua kuwa sasa Umoja wa Ulaya unaendeshwa kwa amri ya Berlin.

Hata hivyo, akitetea kuchaguliwa tena kwa Tusk, Rais Francoise Hollande wa Ufaransa, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Tusk ni alama ya umoja barani Ulaya na kwamba ni yeye aliyependekeza, na sio Ujerumani.

"Lilikuwa ni pendekezo langu kwamba Donald Tusk awe rais wa Baraza la Ulaya. Hakukuwa na sababu ya kupinga chaguo lililofanywa. Tulipaswa kuwa na taswira ya utangamano, utulivu na muendelezo."

Kwa upande wake, Tusk alisema baada ya uchaguzi huo kwamba atashirikiana na wote kwenye utendaji kazi wake, bila kumbaguwa wala kuelemea upande wowote, katika kile kinachoonekana kuwa ni kumjibu waziri mkuu wa nchi yake, Poland.

Awali, Poland ilikuwa imetegemea msaada wa Uingereza wa kutopiga kura yake ili kumkwamisha Tusk, lakini Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, ambaye huu ulikuwa mkutano wake wa mwisho wa kilele, alichukuwa njia ya wanachama wengine 26 kwa kumpigia kura Tusk.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga