1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya Mo Ibrahim 2016 yakosa mshindi

Mohammed Abdulrahman
28 Februari 2017

Wakfu wa Mo Ibrahim umetangaza kwamba hakutokuweko na mshindi wa tuzo yake uongozi bora barani Afrika kwa mwaka 2016. Tuzo ya Mo Ibrahim imepata washindi wanne tu tangu ilipoanzishwa 2006.

https://p.dw.com/p/2YOZK
Mo Ibrahimn
Picha: Barefoot Live

Tangazo hilo lilitolewa Jumanne ( Februari 28 )  kutokana na mkutano  wa kamati  uhuru  ya tuzo hiyo, chini ya Uweyekiti wa Dr Salim Ahmed Salim pamoja na  mkutano wa  bodi ya  wakfu huo uliofanyika  mwishoni mwa juma lililopita.

Akizungumzia juu ya uamuzi wa kamati  ya tuzo hiyo ya Mo Ibrahim, Dr Salim alisema "kama  ninavyosisitiza kila mwaka, paliwekwa kipimo cha hali ya juu, wakati tukizindua tuzo hii  2006.

Tunatambua na  kupongeza mchango muhimu unaotolewa na viongozi wengi wakiafrika kuleta mabadiliko katika nchi zao. Lakini tuzo hii inakusudiwa kumulika na kusherehekea uongozi  wa aina yake, jambo ambalo si la kawaida  ukizingatia kielelezo halisi."

Dr Salim akaongeza kusema kwamba baada ya zingatio makini, kamati hiyo imeamua  kutomzawadia yeyote tuzo hiyo kwa  mwaka 2016.

Mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Mo Ibrahim, Dk. Salim Ahmed Salim (kushoto) amesema kwa mara nyingine hakujapatikana mshindi wa tuzo hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Mo Ibrahim, Dk. Salim Ahmed Salim (kushoto) amesema kwa mara nyingine hakujapatikana mshindi wa tuzo hiyo.Picha: AP

Wagombea wote wa  tuzo ya Ibrahim ni ama viongozi  wa taifa  au Serikali waliondoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliopita  na ambao walikuwa wamechaguliwa kidemokrasi na kutumikia vipindi vyao kwa mujibu wa katiba.

Tangu ilipoanzishwa 2006, tuzo ya Mo Ibrahim imeshatolewa mara nne. Washindi waliopita  ambao wote walikuwa marais wa nchi zao ni, Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Pedro Pires wa visiwa vya Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana  (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2008). Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela alitunukiwa  tuzo ya heshima  2007.

Wakfu wa Mo Ibrahim unatarajia kuwa na  tamasha maalum la "Wikiendi ya Utawala," mjini Marrakech Morocco kuanzia  Aprili 7-9 2017. Tamasha hilo litafunguliwa Ijumaa jioni kwa mjadala wa ngazi ya juu uliopewa jina "Mazungumzo kuhusu  Uongozi", yakizingatia changamoto za  uongozi duniani katika karne ya 21.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / Mtandao wa Mo Ibrahim

Mhariri: Iddi Ssessanga