1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa wana SPD wasubiriwa

Mohamed Abdulrahman13 Desemba 2013

Wengi wa wanachama wa SPD wanatarajiwa kuyaidhinisha makubaliano ya kuunda serikali ya Muungano pamoja na vyama vya kihafidhina CDU na CSU chini ya Uongozi wa Angela Merkel kama Kansela.

https://p.dw.com/p/1AZKa
Matokeo ya kura ya maoni ya wanachama wa SPD kutangazwa Jumamosi.
Matokeo ya kura ya maoni ya wanachama wa SPD kutangazwa Jumamosi.Picha: picture-alliance/dpa

Matokeo ya kura ya wanachama wa chama cha Social Democratic Party kuhusu kujiunga na serikali ya Muungano pamoja na Vyama vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU, yanatarajiwa kutangazwa Jumamosi (14.12.2013). Ikiwa matokeo yataonyesha wanachama wengi wa SPD wanayaunga mkono makubaliano yaliofikiwa kati ya viongozi wao na wahafidhina wakiongozwa na Kansela Angela Merkel, Ujerumani huenda ikawa na serikali mpya mwishoni mwa juma hili.

Kansela Merkel akiwa na Sigmar Gabriel (kushoto) na Horst Seehofer
Kansela Merkel akiwa na Sigmar Gabriel (kushoto) na Horst SeehoferPicha: Reuters

Wengi wanaunga mkono
Utafiti wa kura ya maoni uliochapishwa na kituo cha televisheni cha ZDF jana umeonyesha kwamba 83 asili mia ya walioulizwa kutokana na idadi ya watu 1,255 kwa njia ya simu walisema wanaamini wanachama wa SPD wataidhinisha makubaliano ya kuingia katika serikali ya mseto katika kura hiyo ya maoni. Miongoni mwa wanachama wa SPD 92 asili mia wamesema makubaliano hayo yataungwa mkono.

Tayari makubaliano hayo yameungwa mkono na CDU pamoja na chama ndugu cha Bavaria CSU. Shauku imetanda nchini Ujerumani , huku majina ya watakaokuwemo katika baraza la mawaziri pindi wanachama wa SPD wataamua kuunga mkono makubalino ya kujiunga na serikali ya Muungano, yakiwekwa siri.

Wakati huo huo, hapo mapema Merkel alikutana na Kiongozi wa SPD Sigmar Gabriel pamoja na Horst Seehofer mkuu wa chama cha CSU katika ofisi ya Kansela mjini Berlin. Ingawa hawakuzungumza na waandishi habari, lakini Seefoher ambaye pia ni Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria, alisema hapo kabla kwamba mazungumzo hayo yangehusu uundaji wa Baraza la mawaziri.

Mgawanyo wa wizara
Fununu zilipo ni kwamba huenda Merkel huenda akachukua Wizara tano, tatu kwa chama chake CDU na mbili kwa CSU na kukipa SPD wizara sita katika baraza la mawaziri linalotarajiwa kutangazwa Jumapili. Pamoja na Kansela na katibu wake mkuu, baraza hilo la mawaziri litakuwa na wajumbe 16. Kwa upande wa CDU waziri wa sasa wa Fedha Wolfgang Schaeuble anapewa nafasi kubwa ya kuendelea na wadhifa huo.

Frank-Walter Steinmeier anayetarajiwa kuwa waziri wa nje.
Frank-Walter Steinmeier anayetarajiwa kuwa waziri wa nje.Picha: picture-alliance/dpa

Kulingana na makubaliano, huenda ni vyama vya kisiasa vitakavyoamua vinamteuwa nani. Kiongozi wa SPD Gabriel anapewa nafasi kubwa ya kuwa Waziri wa uchumi na nishati , wakati waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier akitarajiwa kurudi tena katika wadhifa huo, ikiwa utapewa SPD. Steinmeier hata hivyo ana mpinzani katika nafasi hiyo ambaye kiongozi wa wabunge wa SPD Thomas Oppermann.

Uchaguzi wa viongozi wapya
Baada ya matokeo ya kura ya maoni ya wanachama wake 475,000 kutangazwa, wabunge wa SPD watakutana Jumapili mchana, ambapo uchaguzi wa viongozi wapya utafanyika alasiri.

Hali ya mambo inaonyesha Merkel anajiandaa kuingia madarakani kwa mhula wa tatu wa miaka mingine minne ya utawala, hatua iliyofikiwa na makansela wawili tu waliomtangulia wa baada ya vita vya pili, makansela hao ni Helmut Kohl na Konrad Adenauer. Ikiwaitakuwa hivyo basi ataidhinishwa rasmi na bunge Jumanne ijayo.

Muungano wa CDU na CSU ulishinda uchaguzi mkuu Septemba 22 lakini ukapungukiwa na wingi wa kuunda serikali peke yake.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa,afp
Mhariri: Mohammed Khelef