1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubaguzi dhidi ya wanawake bado waendelea

U.Mast-Kirschning - (P.Martin)2 Desemba 2008

Haki za binadamu zinapaswa kutetewa na kuhifadhiwa.Haki hizo hazitetewi tu na mashirika kama Amnesty International na Human Rights Watch,bali huo ni mfumo wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/G7Wf
New UN High Commissioner for Human Rights, South African Navanethem Pillay delivers her speech during the opening session of the 9th UN Human Rights Council at the European headquarters of the United Nations in Geneva, Switzerland, Monday Sept. 8, 2008. (AP Photo/Keystone, Salvatore Di Nolfi)
Mkuu mpya wa Baraza la Haki za Binadamu,Muafrika Kusini Navanethem Pillay.Picha: AP

Tangu Julai mwaka huu,Navanethem Pillay,mwanasheria na mtaalamu wa haki za kiraia kutoka Afrika Kusini ni mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu mjini Geneva Uswisi. Miongoni mwa masuala yanayoshughulikiwa na ofisi hiyo ni vitendo vya kimataifa vinavyoweza kushtakiwa mahakamani,matatizo ya umasikini, ubaguzi,matumizi ya nguvu na vita.Ofisi hiyo hufanya uchunguzi wake wenyewe na hutoa pia mafunzo kuhusu haki za binadamu.

Lakini ubaguzi dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa kabisa katika haki za binadamu.Hayo ni licha ya kuwepo makubaliano mbali mbali ya kimataifa na mchango wa wanawake unaotambuliwa katika maendeleo ya jamii na kuhifadhi amani na usalama.Mwanasheria Pillay alipozungumza mjini Geneva kuadhimisha miaka 60 tangu kutangazwa kwa azimio la haki za binadamu,alisisitiza kuwa ubakaji ni kitendo cha uhalifu kinachopaswa kuadhibiwa.Ubakaji wo wote ule wakati wa vita ni sawa na uhalifu wa vitani.Pasipokuwepo adhabu kali vitendo vya ubakaji vitaendelea katika maeneo ya migogoro kama ilivyo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mtaalamu wa haki za kiraia Pillai amesema,vitendo hivyo vya ukatalii vimekithiri katika maeneo hayo ya mapigano.Makundi yote yenye silaha kuanzia Wakongomani hadi ya kigeni hutumia ubakaji kama silaha dhidi ya wanawake.Maelfu ya wanawake-wazee na hata wasichana wa miezi michache tu ni wahanga wa ubakaji na hakuna hata mtu mmoja alieadhibiwa.Hali hiyo haiwezi kuendelea.

Lakini kama anavyoeleza mwanasheria Pillai,matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake hayatokei katika maeneo ya mapigano tu.Ingawa katika karne iliyopita kumepatikana maendeleo fulani,bado kote duniani na katika jamii zote,matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake na vitendo vya ubakaji hutokea bila ya kuadhibiwa vilivyo kwani mara nyingi hakuna sheria za kutosha.Vile vile mila na tamaduni zingine huchangia matatizo kwani katika jamii hizo wanawake hawathaminiwi sana na hivyo wana haki chache.