1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji yafungua njia ya kusainiwa makubaliano ya CETA

Jane Nyingi
27 Oktoba 2016

Ubelgiji imefanikiwa kutatua mkwamo wake wa ndani uliokuwa kikwazo cha kutiwa saini makubaliano ya biashara huria kati ya Umoja wa ulaya na Canada

https://p.dw.com/p/2RnXa
Symbolfoto europäisch-kanadisches Freihandelsabkommen, CETA
Picha: picture-alliance/K. Ohlenschläger

Hata hivyo mkutano uliokuwa umepangwa kwa hafla ya kutiwa saini makubalino hayo ulikuwa tayari umefutwa kutokana na hofu ya kutopatikana utatuzi wa haraka.Jane Nyingi na ripoti kamili.Kwa muda wa siku kadhaa , serikali ya shirikisho Ubelgiji ilikuwa ikishiriki mazungumzo kujaribu kuushawishi mkoa wa Wallonia kuunga mkono makubalino hayo maarufu kama CETA yanayolenga kuondoa vikwazo vyoyote vya kibiashara ili kurahisisha mtiririko wa bidhaa kati ya Canada na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.Tangazo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu wa mkoa wa Wallonia Paul Magnette "Baada ya mazungumzo ya muda mrefu,hatimae tumefikia makubaliano miongoni mwetu wabelgiji ambayo yatawasilishwa kwa taasisi za umoja wa ulaya na washirika wetu katika umoja huo.Wallonia wamefurahi kuwa matakwa yao yalisikika. Daima tulipigania mikataba ambayo itaimarisha jamii,kanuni za mazingira na kulinda huduma za umma.Wametusikia na hayo yote yatazingatiwa."

Berlin  Protest gegen Handelsabkommen Ceta Symbolbild
Waandamanaji wasiounga mkono CETAPicha: picture-alliance/dpa/J. Carstensen

Mabunge ya maeneo nchini Ubelgiji yana hadi kesho saa sita usiku kuridhia taifa hilo kuidhinisha makubaliano hayo ya CETA. Mataifa wanachama wa EU yamekaribisha hatua hiyo ya Ubelgiji huku waziri wa uchumi hapa ujerumani Sigmar Gabriel akisema wamefanikiwa kuondoa kizuizi kikubwa."Hakuna nchi iliyo karibu nasi kuliko Canada. Canada iko kiulaya zaidi kuliko baadhi ya nchi za bara ulaya, na kwa hivyo nadhani ni hatua nzuri kuanza na Canada, na kujenga kanuni nzuri, kanuni ambazo Marekani haipo tayari kukubaliana nazo. Ndio maana makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani yanayofahamika kama TTIP yamefeli, huku yale ya Canada yakifanikiwa na hivi sasa yatafanyika "alisema waziri huyo wa uchumi.

Slowakei Sigmar Gabriel beim EU-Außenhandelsrates in Bratislawa
Waziri Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/J. Gavlak

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya na maafisa wa Canada lazima pia watathmini nakala ya maelewano yaliyotiwa saini na pande husika nchini Ubelgiji kabla ya kutiwa saini makubaliano hayo ya CETA. Mabalozi wa umoja wa ulaya wanatazamiwa kukutana baadae leo kufuatia kufanikiwa kutatuliwa mkwamo huo. Rais wa baraza la Umoja wa ulaya Donald Tusk nae amezikaribisha habari hizo njema na kusema atasubiri hadi kuondolewa vikwazo vyote kabla ya kuwasiliana na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau.

Makubaliano hayo ya kurahisisha biashara kati ya mataifa ya umoja wa ulaya na Canada yalikuwa yatiwe saini leo katika mkutano uliokuwa ufanyike kati ya EU na Canada mjini Brussels.Baada ya kutoonekana dalili zozote za kupatikana mwafaka ujumbe wa Canada ukiongozwa na waziri mkuu ulivunja safari yake kwenda Ubelgiji na saa chache baadae Umoja wa ulaya ukatangaza kufutiliwa mbali mkutano huo.

Mwandishi:Jane Nyingi/DPAE/AP

Mhariri: Gakuba Daniel