1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubingwa wa Riadha Korea kusini

5 Septemba 2011

Mkuu wa shirikisho la kimataifa la riadha, Lamine Diack, ameyaelezea mashindano ya 13 ya ubingwa wa dunia katika riadha, nchini Korea ya Kusini, kwamba hayakuwa ya kawaida

https://p.dw.com/p/12TOk
Uwanja wa mashindano ya ubingwa wa dunia katika riadha mjini Daegu, Korea KusiniPicha: dapd

Ndivyo ilivyokuwa wakati wengine walikuwa na mwanzo mbaya, kama Mjamaica Usain Bolt, aliyeshindwa kulitetea taji lake katika mbio za mita 100 alipotolewa kwa kuanza vibaya.

IAAF Leichtathletik Weltmeisterschaft Usain Bolt
Usain Bolt wa Jamaica akimaliza mbio za mita 4x100 za kupokezanaPicha: dapd

Hatahivyo, hapo ndipo alipoingiwa na msisimko na huenda ndicho kilichomfanya kuwaongoza wakimbiaji wenzake wa Jamaica kuweka rekodi mpya ya sekunde 37.04 katika mbio za kupokezana za mita 100 mara nne, ikiwa ndiyo zilikuwa mbio za mwisho hapo jana katika kuyakamilisha mashindano hayo ya siku tisa mjini Daegu, Korea Kusini.

Na sio hayo tu, kwani awali Bolt alishinda kwa urahisi fainali za mbio za mita 200 kwa kasi ya sekunde 19.4.

Mwisho wa kwisha mwanariadha huyo anasema ni kweli alikuwa na mwanzo mbaya, lakini alifurahishwa sana na jinsi alivyofanikiwa kuyamaliza mashindano hayo.

Na ufanisi haukuwa kwa Jamaica tu, bali pia ulidhihirika upande wa wanawake, Mkimbiaji Sally Pearson kutoka Australia alipochukuwa ushindi wa mbio za mita 100 kuruka vihunzi na vile vile kwa Mkenya David Rudisha, katika mbio za mita 800 upande wa wanaume, alipoongoza kuanzia mwanzo mpaka kumalizika mbio hizo, na kudhihirisha umahiri wa timu ya Kenya katika safu ya kimataifa.

Commonwealth Games David Lekuta Rudisha
David Lekuta Rudisha wa KenyaPicha: AP

Rudisha pamoja na Wakenya wenzake waliweza kuyamaliza mashindano hayo ya ubingwa wa riadha Korea Kusini wakiwa ni washindani wasio kuwa na upinzani katika mbio za masafa marefu, kuanzia mbio za mita 800 hadi zile za nyika.

Timu pinzani ya jadi ya Kenya, Ethiopia, ikiwa na wanariadha mashuhuri kama Kenenisa Bekele, walishindwa katika ushindani huo.

Kwa jumla, Kenya ilimaliza katika nafasi ya tatu katika wingi wa medali, ikiwa ilijinyakulia medali 17, nyuma ya Marekani iliyokuwa katika nafasi ya kwanza kwa kupokea medali 25, na Urusi katika nafasi ya pili ikiwa na medali 19.

Bolt na kikosi chake kilijizolea medali 9 na ikaanguka katika nafasi ya nne. Ujerumani Ilifuata punde baadaye katika nafasi ya tano, kwa kujinyakulia medali jumla 7.

Hii ni kutokana na mchango wake Matthias de Zordo katika kurusha mkuki, aliyepata medali ya dhahabu akirusha mkuki kwa mita 86.27.

13. IAAF Leichtathletik WM Südkorea Matthias de Zordo Speerwurf
Matthias De Zordo wa UjerumaniPicha: dapd

Naye Robert Harding alipata medali ya dhahabu katika kurusha kisahani, pamoja na David Storl aliyepata dhahabu pia siku ya Ijumaa kwa kurusha kitufe.

Hizo kwa jumla ndiyo dhahabu tatu kwa Ujerumani katika mashindano hayo - zote zikiwa ni katika mashindano ya urushaji.

Ethiopia ilitupwa katika nafasi ya 10 ikiwa na medali 5 pekee.

Mwengine aliyekuwa na ufanisi katika mashindano hayo ni mwanariadha wa Afrika kusini aliyekatwa miguu, Oscar Pistorius, anayetambulika kwa umaarufu kama Blade Runner na alijishindia medali ya fedha katika mbio za kupokezana za mita 100 mara nne baada ya kufuzu kwenye nusu fainali za mita 400.

Mwafrika kusini mwenzake, Castor Semenya, pia aliufurahisha umati kwa mafanikio yake kwa kujishindia pia nishani hiyo ya fedha katika mbio za mita 800 upande wa wanawake, ikiwa anarudi kwenye mashindano hayo baada ya kuandamwa na mzozo wa kijinsia.

Mwenyeji wa mashindano hayo, Korea kusini, iliishia kuwa mwenyeji mwenye matokeo mabaya zaidi katika historia ya mashindano hayo, kwa kushindwa kujinyakulia medali yoyote.

Mwandishi Maryam Abdalla/Rtre/Afpe
Mhariri: Miraji Othman