1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Afghanistan.

Halima Nyanza19 Agosti 2009

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Afghanistan kuondoa agizo lake iliyolitoa la kuzuia vyombo ya habari kuripoti ghasia zitakazotokea katika uchaguzi wa Rais nchini humo utakaofanyika kesho.

https://p.dw.com/p/JEID
Polisi wa Afghanistan wakiwa katika ulinzi mkali, ambapo nchi hiyo kesho inachagua rais mpya.Picha: AP

Ukiipinga amri hiyo iliyotolewa, Umoja wa Mataifa umesema raia wa Afghanistan wana haki ya kupata habari na kwamba kuvizuia vyombo vya habari kunaweza kuondoa imani katika uchaguzi huo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini Kabul Aleem Siddique amesema watu wanahitaji kupewa taarifa sio tu katika siku ya uchaguzi, hata baada ya uchaguzi pia.

Msemaji wa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, amesema wamewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nchi za nje ya nchi hiyo kutaka ufafanuzi au kuondolewa kwa amri hiyo.

Awali Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Afghanistan, Ahmad Zahir amesema amri hiyo ya kutotaka kutangazwa kwa mashambulio hayo wakati wa uchaguzi imetolewa na Baraza la Usalama la Taifa, kwa maslahi ya wananchi wa nchi hiyo.

Amesema vyombo vya habari viko huru kuripoti uchaguzi huo wa kesho Alhamisi, ambapo Wa Afghanistan milioni 17 watapiga kura kuchagua Rais wa nchi hiyo, lakini ripoti kuhusiana na ghasia au mashambulio zimepigwa marufuku.

Ameongeza kuwa hali hiyo siyo ya kawaida na vyombo vyote vya habari lazima vifuate amri hiyo.

Tayari Waandishi wa Habari wa Afghanistan na wa Kimataifa, ambao wameingia nchini humo kuripoti uchaguzi huo, wameripoti kusumbuliwa na hata kupigwa na majeshi ya ulinzi wakati wakijaribu kuripoti matukio kama hayo.

Naye Rais wa Jumuia ya Waandishi huru wa Habari nchini Afghanistan Rahimullah Samander amesema amri hiyo ya kuzuia ni kinyume na katiba na kwamba Waandishi wataidharau amri hiyo, kutokana na kwamba kesho ni siku ya kidemokrasia na ni siku muhimu kwa uhuru wao.

Ubalozi wa Marekani mjini Kabul pia umeikosoa amri hiyo iliyotolewa ya Waandishi kutotakiwa kuripoti mashambulio yatakayofanywa na Taliban wakati wa uchaguzi.

Ikiwa imebaki siku moja tu, kufanyika kwa uchaguzi huo, Kundi la Taliban limeripotiwa kufanya mashambulio ya mfululizo ikiwemo katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul, ambayo wameyaita kama sehemu ya mfululizo wa mashambulio yaliyopangwa kuhujumu hatua ya nchi za magharibi, kuimarisha demokrasia nchini humo.

Aidha Mashambulio hayo yanaonekana kama yamelengwa kuchochea wasiwasi kwa Waafghanistan, kama itakuwa kuna usalama kwao kutoka nje na kwenda kupiga kura, licha ya kuhakikishiwa ulinzi mkali na serikali, ambapo tayari kumeripotiwa mashambulio yalioua wanajeshi watatu wa NATO na Wa Afghanistan wengine wanane wakiwemo wafanyakazi wawili wa Umoja wa Mataifa.

Kwa upande mwingine mmoja wa Waangalizi katika uchaguzi huo wa kesho Jandad Spin Ghar, akizungumzia kuhusiana na uchaguzi huo alikuwa na haya ya kusema.

Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito kwa watu wote wenye uwezo wa kupiga kura kufanya hivyo hapo kesho, kwa lengo la kusaidia ujenzi wa demokrasia nchini humo. na kuwataka wadau wote katika uchaguzi huo kuhakikisha kwamba zoezi hilo linakwenda kama lilivyopangwa.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp)

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman