1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu Togo leo

3 Machi 2010

Wananchi wa Togo leo wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa urais, ambapo kiongozi wa sasa, Faure Gnassinge, anategemewa kushinda kipindi cha pili cha uongozi.

https://p.dw.com/p/MIsB
Rais Faure Gnassingbe wa TogoPicha: DW

Faure ni mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, hayati Gnassingbe Eyadema, ambaye aliongoza Togo bila kupingwa kwa miaka 38.

Wagombea saba wamejitokeza kuwania urais katika uchaguzi huo wa leo, ambao ni moja kati ya chaguzi chache sana za kidemokrasia kuwahi kufanyika katika kipindi cha zaidi ya miongo minne nchini Togo.

Mbali ya Rais huyo wa sasa, Faure Gnassingbe mwenye umri wa miaka 43, wengine ni pamoja na Jean-Pierre Fabre, mwenye umri wa miaka 58 kutoka chama kikuu cha upinzani cha Union of Forces for Change (UFC).Chama hicho kinaongozwa na Gilchrist Olympio ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Togo mara baada ya kupata uhuru.

Fabre ambaye kitaaluma ni mwanauchumi anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Rais Faure Gnassingbe , na hii ni mara yake ya kwanza kuingia katika mbio hizo za kuwania urais.

Mgombea mwengine ni Waziri Mkuu wa zamani, Yawovi Agboyibo,kutoka chama cha Action Committee for Renewal (CAR), hii ikiwa ni mara yake ya tatu kujaribu bahati ya kuingia Ikulu.Aliwahi kushiriki katika chaguzi mbili bila ya mafanikio mwaka 1998 na 2003.

Mwengine ni Waziri Mkuu wa zamani pia, Messan Agbeyome Kodjo, anayekiwakilisha chama cha Organisation for the Building of a United Togo, OBUTS, kwa ufupi.Kodjo alijiondoa kutoka chama tawala cha Togolese People's Rally (RPT) mwaka 2005 na kuanzisha chama chake.

Kodjo mbali ya kuwa waziri mkuu, pia amewahi kuwa spika wa bunge la Togo kuanzia mwaka 1999 hadi 2000, huku hapo kabla akishika nafasi kadhaa za uwaziri katika serikali ya hayati Rais Gnassingbe Eyadema. Hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika mbio hizo za kwenda Ikulu.

Mwanamke pekee aliyejitokeza kuwania urais wa Togo katika uchaguzi huo wa leo, ni Brigitte Kafui Adjamagbo-Johnson kutoka chama cha Democratic Convention of African Peoples .Ana shahada ya juu katika sheria.

Hata hivyo, Rais wa sasa Faure Gnassingbe anaonekana kuwa nafasi nzuri ya kushinda tena muhula wa pili, kutokana na kile upinzani unachosema kuwa, vitendo vya wizi wa kura na hila nyingine vikimsaidia.

Kumekuwa na taarifa kuwa majina ya wapiga kura yameshafanyiwa hila katika eneo la Kusini mwa Togo.

Jean-Pierre Fabre mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha UFC anaonya juu ya hilo.

´´Hakuna mtu ambaye anataka kuona ushaguzi ambao matokeo yake tayari yamekwishajulikana hata kabla ya kura kupigwa.Chama tawala cha RPT kitashindwa katika uchaguzi lakini bado hata hivyo kitatangaza kuwa kimeshinda.Na hilo kamwe hatutoruhusu litokee.Hii ni hatari kwasababu inaweza kusababisha ghasia´´

Hata hivyo Rais Faure amesema kuwa atahakikisha uchaguzi huo wa leo unakuwa huru na wa haki na kwamba hakuna mtu atakayepata mwanya wa kufanya ghasia.

´´Sitoonyesha udhaifu katika kuwashughulikia wale watakaojaribu kuleta fujo, wakati wa kupiga kura au baada ya uchaguzi´´

Uchaguzi uliyopita nchini Togo uligubikwa na ghasia za kupinga matokeo yaliyomuweka madarakani kiongozi huyo, ambapo inakadiriwa kiasi cha watu 800 walipoteza maisha.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mpitiaji:Othman Miradji