1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo; maoni ya Ute Schäffer

30 Oktoba 2006

Kura zimeanza kuhesabiwa katika raundi ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Rais wa sasa Joseph Kabila anataziwa kumshinda mpinzani wake Jean Pierre Bemba. Jee mahasimu hao wataheshimu matokeo ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/CHLH



Kura zimeanza kuhesabiwa katika raundi ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Matokeo yanasubiriwa kwa hamu kubwa !

Iwapo matokeo hayo yatajenga msingi wa amani nchini JJK itafahamika hapo baadae. Mtu mmoja amekufa kufuatia ghasia zilizosababishwa na madai juu ya udanganyifu. Lakini kutokana na kuwapo nchini humo, majeshi ya nchi za Ulaya,na ya Umoja wa Mataifa ghasia hizo hazikuweza kupamba moto.

Bila ya msaada wa jumuiya ya kimataifa isingewezekana kwa JKK kuandaa na kufanya uchaguzi huo. Wakati wote ni wasuluhishi wa kimataifa waliowaleta pamoja wapinzani wakuu katika uchaguzi huo, rais wa sasa bwana Joseph Kabila na makamu wake bwana Jean Pierre Bemba. Mahasimu hao wameweza kufikia usikizano kutokana na juhudi za wasuluhishi wa kimataifa.

Swali la kuuliza sasa,ni nini kinaweza kutokea ikiwa majeshi ya nchi za Ulaya yataondoka nchini JKK?

Jumuiya ya kimataifa imetoa mchango mkubwa katika mchakato wa kisiasa nchini humo. Pamekuwapo mikutano kem kem ya kimataifa katika ngazi mbalimbali. Harakati hizo zinaonesha jinsi nchi hiyo inavyotiliwa maanani na jumuiya ya kimataifa. Hivyo basi litakuwa kosa kubwa ikiwa ,uwalikishi wa jumuiya ya kimataifa utamalizika mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.!

Yafaa kukumbuka kwamba rais Kabila pamoja na mpinzani wake bwana Bemba, wamejijenga kisiasa kutokana na harakati za kijeshi kwa usemi mwingine kutokana na kutumia mabavu.

Hivyo basi mshindi wa uchaguzi atabakia kuwa mwanajeshi na siyo raia.

Hivyo suala la kutilia maanani ni iwapo atakaeshinda ataweza kudumisha amani, kwani nchi hiyo ina makundi yenye maslahi tofauti. Jee atakaechaguliwa kuwa rais ataweza kuyanyamazisha makundi hayo kwa njia ya amani?

Yeyote atakechaguliwa kuiongoza JKK atakabiliwa na changamoto kubwa.

Mapato yanayotokana na raslimali za nchi lazima yahalalishwe, ili yaingie katika bajeti ya nchi, makundi ya waasi lazima yadhibitiwe, mamilioni ya silaha zilizotapakaa nchini kote ,kadhalika lazima zikusanywe. Pamoja na hayo pana changamoto ya kulijenga upya jeshi lisilokuwa na nidhamu.

Rais wa sasa bwana Kabila na mpinzani wake hawajaonesha dalili za kuwa tayari kufikia usikizano. Kauli walizokuwa wanatoa katika kampeni za uchaguzi ziliashiria uadui, chuki na hata ukabila.

Atakaeshinda pia atakabiliwa na changomoto ya watu wanaonufaika na utajiri wa nchi hivi sasa: kudumishwa kwa amani kutamaanisha kupotea kwa mapato ya watu hao.

Amani nchini JKK ni muhimu kwa eneo zima la afrika ya kati na ya mashariki.

Hivyo basi utakuwa uamuzi wa busara ikiwa angalau Umoja wa Mataifa utaendelea kuwapo nchini humo hata baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa rasmi.

Imetafsiriwa na Abdu Mtullya.