1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Uingereza waitia kiwewe EU

Admin.WagnerD5 Mei 2015

Uchaguzi mkuu wa Uingereza unakuja na hatari kubwa, si tu kwa siasa za ndani ya Uingereza, lakini pia bara la Ulaya kwa ujumla: Baadhi wanahofu kuwa kura hiyo inaweza kuwa mwanzo wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1FKXf
Britischer Premier Cameron stellt Wahlprogramm vor
Picha: Reuters/T. Melville

Wakati wapigakura watakapoelekea vituoni Alhamisi wiki hii (Mei 8), wanasiasa wa nchi hiyo hawatakuwa pekee watakaosubiria matokeo ya mwisho kwa wasiwasi. Hali ya mashaka itatawala barani Ulaya kote pia, kukiwa na wasiwasi kwamba kile kinachojulikana kama "Brexit" kinakaribia.

Neno hilo lililotungwa kuelezea uwezekano wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya - limekuwa likisikika mara kwa mara mjini Brussels, yaliko makao makuu ya umoja huo, tangu waziri mkuu wa Uingereza David Cameron alipoahidi kuitisha kura ya maoni juu ya uanachama wa Umoja wa Ulaya, ikiwa chama chake kitashinda uchaguzi mkuu wa mwezi huu.

Michael Emerson, kutoka kituo cha ushauri juu ya masuala yanayohusiana sera ya Ulaya, alisema uundwaji wa serikali ijayo unaweza kuwa tu mwanzo wa mashaka. " Kuondoka kwa Uingereza kunaweza kusababisha uharibifu usiyoelezeka kwa ukamilifu na uaminifu wa Umoja wa Ulaya, aliongeza mchambuzi wa kituo cha Carnage Europe Jude Dempsey, na kusema kuwa Cameron ameiweka Uingereza kwenye njia ya msuguano na washirika wake wa Ulaya, jambo alilolitaja kuwa hatari.

Wagombea wa upinzani wakiwa katika mjadala wa televisheni.
Wagombea wa upinzani wakiwa katika mjadala wa televisheni.Picha: AFP/Getty Images/S. Rousseau

Kiini cha mizozo na malumbano

Lakini Cameron hajawahi kuona haya kuutikisa Umoja wa Ulaya. Katika miaka michache iliyopita, amekuwa kiini cha wasiwasi na malumbano kuhusu kila kitu, kuanzia bajeti za jumuiya hiyo, hadi kwenye nfasi za juu za ajira, uhamiaji na sheria mpya kuhusu nidhamu ya fedha. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Waingereza ni watu wasioupenda Umoja wa Ulaya, licha ya kuwa wanachama wa jumuiya hiyo kwa zaidi ya miaka 40.

Alipotoa ahadi ya kuitisha kura ya maoni mwaka 2013, Cameron aliapa kuanza kujadili makubaliano mapya, na Umoja wa Ulaya juu ya mabadiliko zaidi na uwajibikaji wa kidemokrasia, na vile vile mamlaka zaidi ya kitaifa. Alisema watakapojadili makubaliano mapya, atawapa raia wa Uingereza kura ya maoni kwa chaguo rahisi la aman kuendelea kubakia au kutoka.

Lakini Cameron anakabiliwa na njia ngumu hapo mbele, kuwashawishi wenzake 27 wa Umoja wa Ulaya kukubaliana na mpango wake wa majadiliano mapya. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye mara nyingi huonyeshwa kama kiongozi mwenye nguvu zaidi wa kitaifa katika Umoja wa Ulaya, aliondoa matumaini ya kuzifanyia mageuzi makubwa kanuni za msingi wa umoha huo tangu mapema mwaka jana.

Katika hotuba yake kwa mabaraza ya bunge la Uingereza mwaka uliyopita, Merkel alisema na namnukuu: Baadhi wanategemea hotuba yangu kusafisha njia kwa mageuzi makubwa ya miundombinu ya Umoja wa Ulaya, ambayo yatakidhi aina zote za matakwa ya Uingereza. Nahofia kwamba watakatishwa tamaa, mwisho wa kunukuu.

Kiongozi wa chama kinachoupinga Umoja wa Ulaya na uhamiaji Nigel Farage amekuwa akiwaumiza vichwa Conservatives.
Kiongozi wa chama kinachoupinga Umoja wa Ulaya na uhamiaji Nigel Farage amekuwa akiwaumiza vichwa Conservatives.Picha: Getty Images/Carl Court

Hofu ya mwadhara makubwa

Lakini pia alikataa kusema kwamba mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya hayako tayari kulipa gharama yoyote ili kuibakiza Uingereza katika umoja huo. " Uingereza ni sehemu ya EU," alisisitiza msemaji wa Merkel Steffen Seibert Juni mwaka jana. Jumuiya hiyo, ikikabiliana na athari mbaya za mgogoro wa kiuchumi na changamoto za kisiasa kwenye mataifa ya mashariki na kusini, iko makini kuendeleza umoja na mshikamano.

Watetezi wa uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya wanasema pia nchi hiyo haiwezi kuendelea kuwa na ushawishi wa kimataifa ikiwa pekee yake, kusimama dhidi ya mataifa makubwa kama Urusi na China, au uhalifu unaovuka mipaka kama vile ugaidi. Wachambuzi wanasema hata ishara tu kwamba nchi hiyo inaweza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, inaweza kuiathiri sekta ya fedha ya taifa hilo, kutokana na muingiliano mkubwa wa kifedha na kiuchumi, uliyopo kati ya Uingereza na matiafa mengine ya Ulaya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae
Mhariri: Josephat Nyiro Charo